Habari Mseto

Ruto awaonya wanasiasa dhidi ya kutumia BBI kupanda mbegu za migawanyiko nchini

December 16th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ameshauri wanasiasa kukoma kutumia mchakato wa maridhiano (BBI) kuwagawanya Wakenya.

Aliwakata viongozi wa kisiasa kuwaruhusu Wakenya kuchambua mageuzi ya katiba yaliyopendekezwa kwa njia huru ili wafanye maamuzi kwa njia huru bila kuelekezewa vitisho.

Akiongea katika Kaunti ya Narok Jumatano, Dkt Ruto pia aliwataka viongozi kuendesha elimu kwa umma kuhusu sehemu kadha katika ripoti hiyo badala ya kuendesha kampeni za NDIO au LA ambazo zitalenga migawanyiko miongoni mwa Wakenya.

“Mageuzi ya Katiba hayafai kutumiwa kuleta migawanyiko na uhasama miongoni mwa Wakenya. Hawafai kuwatia woga na kuwawekea Wakenya matakaa fulani,” akaeleza.

Dkt Ruto alikuwa akiongea Jumatano alipohudhuria mazishi ya Nalangu Enole Ntutu, mamake aliyekuwa Seneta wa Narok Stephen Ole Ntutu na Waziri Msaidizi wa Leba Patrick Ole Ntutu, nyumbani kwa Ololunga, eneo bunge la Narok Kusini.

Naibu Rais alikuwa ameandamana na Waziri wa Leba Simon Chelugui, Magavana Samuel Tunai (Narok), Hillary Barchok (Bomet) na Joseph Ole Lenku (Kajiado), na wabunge Korei Ole Lemein (Narok Kusini), Soipan Tuya (Mbunge Mwakilishi, Narok) and David Ole Sankok (Mbunge Maalum).

Wabunge wengine walikuwa; Johana Ng’eno (Emurua Dikirr) Ndindi Nyoro (Kiharu) na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki).

Kwa mara nyingine Dkt Ruto alishikilia kuwa bado ipo nafasi ya kufanyia mageuzi mswada wa BBI ili kushirikisha maoni ya makundi mbalimbali yasioridhika.

Kauli yake ilionekana kukinzana na ile ambayo Rais Uhuru Kenyatta alitoa wakati wa sherehe za Jamhuri Dei alipowataka wanaopinga mswada wa BBI kutovunjika moyo kwani watapata nafasi ya kuwasilisha mapendekezo yao wakati wa awamu ya pili ya mageuzi ya Katiba.