Habari

Ruto awapongeza washindi wa chaguzi ndogo Ugenya, Embakasi Kusini

April 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU RAIS  William Ruto, Jumamosi ametuma ujumbe wa pongezi kwa washindi katika chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini zilizofanyika Ijumaa.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter Naibu Rais amesema ushindi wa Julius Mawathe (Wiper) katika eneobunge la Embakasi Kusini na David Ochieng’ (MDG) katika eneobunge la Ugenya ni ishara kwamba raia wa kawaida wana uwezo wa kuhakikisha sauti yao inasikika kisiasa bila kuyumbishwa na wanasiasa.

David Ochieng’ wa chama cha MDG alipohutubia wanahabari baada ya IEBC kumuidhinisha rasmi kuwania ubunge eneobunge la Ugenya katika hii picha ya Februari 4, 2019. Picha/ Tonny Omondi

“Pongezi Ochieng (Ugenya) na Mawathe (Embakasi) kwa ushindi wenu ambao umeletwa na Mungu. Huu ni usemi wa mahasla, uamuzi wa wananchi. Jina la Mungu litukuzwe,” Dkt Ruto akasema.

Katika matokeo yaliyotangazwa usiku wa kuamkia Jumamosi Bw Ochieng’ alishinda kwa kupata kura 18,730 na kumshinda mgombea wa ODM Christopher Karan aliyepata kura 14,507.

Na katika eneobunge la Embakasi Kusini Bw Mawathe aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 21,628 huku mgombea wa ODM Irshad Sumra akipata kura 7, 988 pekee.

Ushindi wa Ochieng’ umefasiriwa kuwa pigo kubwa sio tu kwa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga bali Seneta wa Siaya James Orengo ambaye ni mzaliwa wa eneobunge hilo.

Isitoshe, mwanasiasa huyo ambaye alipania kutumia ushindi huo kama ngazi ya kumwezesha kuwania ugavana wa Siaya 2022, amewahi kuhudumu kama mbunge wa Ugenya kwa zaidi ya miaka 20.

Changamoto

Hata hivyo, ni idadi ndogo mno ya wapigakura waliojitokeza vituoni katika maeneobunge ya Embakasi Kusini na Ugenya.

Watu watatu walikamatwa na polisi na kushtakiwa kortini huku mmoja akilazwa hospitalini ghasia zilipozuka kwenye uchaguzi mdogo wa Ugenya, wafuasi wa vyama vya ODM na MDG walipozozana na kupigana.

Vilevile, palishuhudiwa matatizo ya mitambo katika vituo kadhaa vya kupigia kura, wakati mashine hizo zilipokosa kutambua wapigakura kwa kutumia vidole, hali ambayo ilitatiza shughuli hiyo kwa muda.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati na Afisa wa kusimamia uchaguzi Ugenya Vincent Saitabau, walikiri kuwa palikuwa na changamoto, lakini wakasema zilirekebishwa baada ya muda mfupi.

Aidha, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji aliamrisha mgombea wa chama cha ODM katika eneobunge la Ugenya Christopher Karan ashtakiwe, baada ya kubainika kuwa alighushi barua katika kesi ya uchaguzi dhidi yake na mshindani wake David Ochieng’.

Amri iliyochapishwa kwenye gazeti la serikali ilisema Bw Karan alighushi barua kudai kuwa alikuwa hospitalini, alipochelewa kuwasilisha majibu ya kesi kortini.

Bw Karan alilalamika kuwa wafuasi wake walivamiwa na mmoja akakatwa, huku wapinzani wake wakilalamika kuhusu hitilafu za mitambo ambazo zilisitisha zoezi hilo.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, wakazi waliwahi mapema katika vituo vya kupigia kura, huku washindani wakuu Irshad Sumra na Julius Mawathe wakishiriki shughuli hiyo pamoja na wafuasi wao.

Bw Chebukati ambaye alikagua baadhi ya vituo vya kupigia kura alisema shughuli hiyo iliendelea kwa njia shwari.

Wapigakura waliozungumza na Taifa Leo walisema shughuli hiyo ilikuwa likiendeshwa kwa kasi nzuri, licha ya hitilafu ndogo ambazo zilishuhudiwa mwanzoni.

Aidha Bw Karan na Bw Mawathe walipoteza viti vyao kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu, kuhusiana na utata ulioshuhudiwa katika uchaguzi wa Agosti 2017.

Hata hivyo, Mawathe amehifadhi kiti chake huku Karan akipoteza.