Ruto awataka machifu waliotekwa na wanasiasa warejee kazini

Ruto awataka machifu waliotekwa na wanasiasa warejee kazini

NA SAMMY WAWERU

RAIS Mteule Dkt William Ruto amewataka machifu na watumishi wa umma waliokuwa wameshikwa mateka na wanasiasa kuwafanyia kampeni, warejee kazini ili watekeleza majukumu yao.

Dkt Ruto amekuwa akidai baadhi ya machifu wamekuwa mateka wa mrengo fulani wa kisiasa, kuutafutia kura.

Amesema Jumatano watumishi wa umma hawapaswi kushiriki siasa, na badala yake wanatakiwa kuhudumia umma.

Akihutubu Karen, jijini Nairobi baada ya kukutana na wajumbe waliochaguliwa kupitia vyama tanzu vya Kenya Kwanza, alisisitiza watumishi wa umma wanapaswa kutekeleza wajibu wao bila kuegemea upande wowote wa kisiasa.

“Kwa waliotumika kisiasa hasa machifu, warejee kazini kutekeleza majukumu yao…Wakenya wanataka maendeleo,” Dkt Ruto akasema.

“Watumishi wa umma tunatarajia mfanyie wananchi kazi bila mapendeleo,” akasisitiza.

Wakati akifanya kampeni kusaka urais, Dkt Ruto alikuwa akilalamikia machifu na wakuu wa polisi kutumiwa na serikali kufanyia kampeni wapinzani wake.

Katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9, 2022, Ruto alimenyana na kinara wa Azimio, Bw Raila Odinga.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilimtangaza rasmi kuwa mshindi. Bw Odinga hata hivyo amepuuzilia mbali matokeo hayo.

Ruto amehudumu kama naibu wa rais kati ya 2013 – 2022, na amekuwa akiteta kutengwa serikalini hasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Odinga kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa 2018 kupitia salamau za maridhiano, Handisheki.

“Siasa zitekelezwe na wanasiasa. Watumishi wa umma wafanye kazi zao,” akasema.

Dkt Ruto hata hivyo amehakikishia waliokuwa wameshikwa mateka kisiasa, nafasi zao za kazi ni salama na kwamba hawatamwaga unga.

  • Tags

You can share this post!

Muffins za karoti na zisizo na mayai

Kipa Opiyo akubali mkataba mpya kuchezea Ingwe

T L