Ruto ikulu katika jaribio la kwanza

Ruto ikulu katika jaribio la kwanza

NA BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto ameweka historia kwa kuwa mwanasiasa wa kwanza nchini Kenya kugombea urais mara ya kwanza na kuibuka mshindi.

Dkt Ruto pia ndiye naibu wa rais wa kwanza nchini kugombea urais na kushinda katika jaribio lake la kwanza.

Ushindi huo hata hivyo umepingwa na kinara wa mrengo pinzani wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga ambaye ameapa kuelekea mahakamani kupinga ushindi huo.

Bw Odinga amegombea urais mara tano na hajawahi kutangazwa mshindi.Bw Odinga amekuwa akigombea urais tangu 1997 isipokuwa 2002, alipomuunga mkono Mwai Kibaki aliyemshinda Uhuru Kenyatta wa chama cha Kanu kuwa rais wa tatu wa Kenya.

Dkt Ruto aliyepata kura 7,176, 141 dhidi ya 6,942,930 za Bw Odinga ndiye naibu wa rais kwa kwanza kurithi urais kutoka kwa mkubwa wake baada ya kushinda uchaguzi mkuu.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa, ushindi wa Dkt Ruto umetokana na mikakati yake thabiti ya kisiasa, uwezo wake wa kifedha na mtandao wa washirika ambao amejenga nchini kwa miaka ambayo amekuwa mwanasiasa na serikalini.

“Ukakamavu wake, nguvu, ujasiri na uzoevu ambao amepata chini ya marais watatu aliohudumu chini yao, Moi, Kibaki na Kenyatta umemwezesha kujenga mtandao wa washirika kote nchini, jambo ambalo ni muhimu kwa siasa,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Nicholas Rotich.

Anasema kwamba, Dkt Ruto hawezi kufananishwa na makamu rais wa zamani walioshindwa katika majaribio ya kwanza ya kugombea urais baada ya kuondoka mamlakani kama vile Kibaki na Mudavadi.“Mazingira ni tofauti kabisa na wapigakura pia ni tofauti,” asema.

Dkt Ruto amepanda ngazi kutoka kijana wa kawaida kijijini hadi sasa anaposubiri kuapishwa kukalia kiti kikubwa zaidi katika taifa la Kenya.

“Hapa nilipofika ni Mungu. Ninaweza kuthibitisha tumeombewa kuwa washindi,” Dkt Ruto alisema baada ya kupokezwa cheti cha ushindi na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati, Jumatatu jioni.

Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi aliingia mamlakani kufuatia kifo cha rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta mwaka wa 1978 baada ya kuwa makamu rais kwa miaka 13.

Kabla ya uchaguzi wa 2002 ambao upinzani uliungana dhidi ya chama tawala cha Kanu, Kibaki alikuwa amegombea urais mara tatu bila kushinda.

Aligombea urais mara ya kwanza mwaka wa 1992 siasa za vyama vingi ziliporuhusiwa nchini.

Rais Mteule, William Ruto akihutubia viongozi waliochaguliwa chini ya Kenya Kwanza katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi, Agosti 17, 2022. PICHA | JEFF ANGOTE

Kabla ya siasa za vyama vingi, Kibaki alikuwa amehudumu kama makamu wa rais wa Rais Moi.

Rais Uhuru Kenyatta alishinda urais kwenye uchaguzi wa 2013 katika jaribio lake la pili baada ya kushindwa na Kibaki mnamo 2002.

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka hakufaulu alipogombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2007, naye kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi alishindwa kwenye jaribio lake la kwanza mnamo 2013.

Bw Mudavadi na Bw Musyoka wamewahi kuwa makamu rais katika vipindi tofauti nchini.

Wanasiasa wengine ambao wamewahi kugombea urais bila kufaulu ni kiongozi wa chama cha National Rainbow Coalition (Narc) Bi Charity Ngilu ( (1997), mwenzake wa Narc Kenya Bi Martha Karua (2013) na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth (2013).

  • Tags

You can share this post!

Azimio wasisitiza kuwa mapambano yataendelea

Rigathi Gachagua sasa ataka Uhuru avunje kimya chake

T L