Ruto azidi kuhusishwa na kesi ya ICC

Ruto azidi kuhusishwa na kesi ya ICC

NA VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto, amezidi kutajwa katika kesi dhidi ya wakili Paul Gicheru, aliyeshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa madai ya kushawishi mashahidi wajiondoe kwa kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Huku mahakama ikitarajiwa kupokea hotuba za mwisho za pande husika katika kesi hiyo wiki ijayo, upande wa mashtaka umesisitiza kuwa, Bw Gicheru alikuwa mwandani wa Dkt Ruto na alitumia vitisho na hongo kuwafanya mashahidi wasishirikiane na ICC.

Katika nakala ya hoja zinazotarajiwa kuwasilishwa kortini wiki ijayo, upande wa mashtaka umedai kuwa mmoja wa mashahidi alifichua hofu yake kuwa Dkt Ruto angemwangamiza endapo angeendelea kutoa ushahidi dhidi yake kuhusu ghasia hizo.

Upande wa mashtaka pia umeeleza kuwa ushahidi uliokusanywa kutoka kwa uchunguzi wa simu za baadhi ya mashahidi na zile za Bw Gicheru, ulimhusisha Dkt Ruto na sakata ya kushawishi mashahidi wajiondoe kwenye kesi dhidi yake.

Imedaiwa kuwa Naibu Rais alipokuwa akiendeleza njama hizo, aliwaficha mawakili wake wakuu kuhusu yaliyokuwa yakiendelea.

Kikosi cha mawakili wake kiliongozwa na Bw Karim Khan, ambaye sasa ni kiongozi wa mashtaka wa ICC.

Kabla ya kuapishwa kwake kuchukua mahali pa Bi Fatou Bensouda aliyekamilisha hatamu yake kama kiongozi wa mashtaka, Bw Khan alikula kiapo kwamba hatajihusisha katika kesi yoyote ambayo huenda akaonekana kuwa na mapendeleo kuihusu.

Bw Gicheru alishtakiwa kwa madai kuwa alitekeleza mambo kama vile kuwasaka, kuwatishia na kuwahonga baadhi ya mashahidi kwa mamilioni ya pesa ili wajiondoe katika kesi hizo kwa niaba ya Dkt Ruto.

“Hatua zilizochukuliwa na Gicheru kuepuka kupatikana ni kama vile kukataa kunakili makubaliano na mashahidi waliohongwa, kutumia pesa taslimu kuwahonga mashahidi ili kuepuka rekodi za benki, kuwaagiza mashahidi wasipeleke pesa walizopewa katika benki na kuhakikisha wakili mkuu wa Ruto hakujua kuhusu njama hizo,” upande wa mashtaka unaeleza.

Hata hivyo, katika nakala anayonuia kutumia kwa utetezi wake, Bw Gicheru amesisitiza kuwa hana hatia yoyote huku akilaumu upande wa mashtaka kwa kutumia uvumi katika kesi zinazohusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kupitia kwa wakili wake, Bw Michael Karnavas, amesema masuala yote yaliyotajwa dhidi yake na upande wa mashtaka ni uongo mtupu kwa hivyo mahakama inafaa iamue kwamba hana hatia.

Kulingana naye, baadhi ya mashahidi walioitwa hawawezi kuaminika. Anadai kuwa mashahidi wengi walikuwa wamekubali kushirikiana na ICC tu kwa kuwa waliahidiwa kuhamishwa ili wakaishi ughaibuni ambapo wengine wao walivutiwa na matarajio ya maisha bora kuliko yale walikuwa wakiishi Kenya.

“Upande wa mashtaka haukufanya upelelezi wowote Rift Valley. Majasusi hawakuzuiwa na serikali ya Kenya kufanya uchunguzi huko, lakini kutokana na uamuzi wao wenyewe wa kutofanya upelelezi Rift Valley, wapelelezi hawakuwahi kutembelea maeneo yanayodaiwa yalitendewa uhalifu ili wajifanyie uchunguzi huru,” akasema Bw Karnavas.

Wengine wanaodaiwa walihusika kwa njama za kuvuruga mashahidi ni Silas Kibet Simatwo ambaye alikuwa katika bodi ya kampuni ya bima ya Amaco inayohusishwa na Dkt Ruto, Isaac Maiyo aliyekuwa mwenyekiti wa CDF Eldoret Kaskazini, marehemu Meshack Yebei ambaye alipatikana ameuawa na mwili wake kutupwa katika mbuga ya wanyama, Philip Kipkoech Bett aliyekuwa mwanaharakati katika shirika la Kalenjin Youth Alliance, na mwanahabari Walter Barasa.

ICC ilikuwa imetoa agizo la kukamatwa kwa Mabw Bett na Barasa.

Wengine ni Elisha Kipkorir Busienei, mwanachama wa ODM ambaye baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Turbo, na baadhi ya mashahidi wa awali waliobadili misimamo na kuamua kushirikiana na wandani wa Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Aliyenaswa na silaha kujua hatima yake leo Ijumaa

Droo ya Dala Sevens yatangazwa, KCB na Strathmore kufufua...

T L