Habari MsetoSiasa

Ruto azidi kutumia Twitter kupinga mabadiliko katika chama cha Jubilee

April 15th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto Jumanne jioni aliendelezea mvutano wa uongozi ndani ya chama tawala cha Jubilee kwa kudai kuwa jumla ya wabunge na maseneta 146 wanapinga mabadiliko yaliyofanywa katika kamati ya uongozi wa chama hicho.

Kwenye taarifa katika akaunti yake ya Twitter Dkt Ruto anadai kuwa viongozi hao wanapinga mabadiliko hayo yaliyotekelezwa na Katibu Mkuu Raphael Tuju na ambayo alitaja kama haramu.

Miongoni mwa wabunge ambao Dkt Ruto alidai wanapinga mabadiliko hayo ni kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale, mwenzake wa Seneti Kipchumba Murkomen, Naibu Katibu Mkuu Caleb Kositany na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

“Asilimia 70 ya wabunge na maseneta waliochaguliwa, yaani wajumbe 146, wamekaa njama na jaribio haramu ya mabadiliko yanayotekelezawa na majambazi wanajificha katika janga la corona linalowakumba Wakenya. Hawa sio watu wa Rais Uhuru Kenyatta. Hawa ni majangili wenye nia ya kuvuruga chama chetu cha Jubilee,” akasema Dkt Ruto.

Katika ilani iliyochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali mnamo Aprili 6, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alitangaza nia ya chama cha Jubilee kubadili wanachama wa Kamati ya Simamizi ya Kitaifa (NMC) ya Jubilee. Wanachama wapya waliopendekezwa kuwa wanachama wa kamati hiyo ni; Lucy Nyawira Macharia, Profesa Marete Marangu, aliyekuwa Mbunge wa Kitutu Masaba Walter Nyambati, Jane Nampaso na James Waweru.

Dkt Ruto ambaye ni naibu kiongozi wa Jubilee alipinga hatua sawa na wabunge kadhaa wanaounga mkono azma yake ya kuingia Ikulu 2022. Naibu Rais aliamwandikia barua Bi Nderitu mnamo Ijumaa Aprili 10, 2020 akipinga mabadiliko hayo, alisema ni haramu kwamba hayakuidhinishwa na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya Jubilee.

“Nimeona notisi katika gazeti rasmi la serikali….. ambapo inadaiwa kuwa mabadiliko yamefanywa katika uanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ya chama cha Jubilee. Tafadhali fahamu kwamba kamati ya NMC haijafanyiwa mabadiliko na chama kupitia Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) inavyohitajika kwa mujibu wa katiba yetu. Kwa hivyo, mabadiliko yanayonuiwa kufanywa kwa kamati ya NMC, ni haramu na yanasheheni ulaghai mkubwa,” Dkt Ruto.

Akijitetea, Bw Tuju alisema kuwa mabadiliko hayo yalitekelezwa baada ya baadhi ya waliokuwa wakishikilia nyadhifa hizo kupata kazi serikalini.

“Barua ya kupendekeza mabadiliko hayo iliandikiwa mnamo Machi 23 na kelele zinazotolewa kuhusu majibu ya msajili wa vyama vya kisiasa hayana maana, “ akasema Bw Tuju.

Kwa upande wao, wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto wanadai kwua mabadiliko hayo yanalenga kumfurushwa Naibu huyo wa Rais kutoka chama cha Jubilee.