Habari

Ruto azima uvumi kuhusu alikokuwa amekwenda

November 22nd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MASWALI kuhusu alikozuru Naibu Rais William Ruto yalipata majibu baada kiongozi huyo kufichua Jumamosi yuko Dubai.

Ingawa hakufafanua shughuli iliyompeleka huko, Dkt Ruto alisema yuko ziarani Dubai ambako ameandamana na Seneta wa zamani wa Mombasa Omar Hassan.

“Jioni ya leo nilitangamana na Hasla Salt Bae, muuzaji nyama raia wa Uturuki, ambaye ameinuka kibiashara baada ya kuanza kuuza chumvi, nyama na kisu,” akaandika kwenye akaunti yake ya Twitter.

Nusret Gokce, almaarufu Salt Bae, ni mpishi na mfanyabiashara maarufu wa mikahawa ambaye anamiliki biashara hizo katika miji 16 kote ulimwenguni, ikiwemo Dubai ambako Dkt Ruto alitembelea.

Naibu Rais vile vile alitumia fursa hizo kuwasilisha ujumbe kwa wafuasi wake, maarufu kama “Hustler Nation” akiwahimiza kuendelea kujizatiti kujiimarisha kupitia biashara zao ndogondogo.

“Mahasla wa Kenyatta, Burma na Dagoretti na wengine mko na ushindani na kitu cha kujifunza hapo; mjipange. Kazi ni kazi,” Dkt Ruto akaandika.

Ujumbe na Naibu Rais ulitokana na makisio mengi yaliyotanda katika mitandao ya kijamii kuhusu alikokuwa ameenda na hali yake ya kiafya siku za Ijumaa na Jumamosi.

Kando na Dkt Ruto, maswali pia yaliibuliwa kuhusu alikokwenda kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye “alitoweka” siku moja baada ya kuahirishwa kwa shughuli ya ukusanyaji sahihi za kuidhinishwa mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia mapendekezo ya ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI).

Baadaye iliibuka kuwa Bw Odinga alikuwa amesafiri kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika wadhifa wake kama Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundonsingi.

Viongozi hao wawili wamekosa kusikika tangu Jumatano jioni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuahirisha shughuli ya uzinduzi wa ukusanyaji wa sahihi za BBI dakika za mwisho.