Habari

Ruto azimwa huku Raila akiandaliwa zulia jekundu katika mikutano ya kisiasa

October 10th, 2020 2 min read

RUTH MBULA na FADHILI FREDRICK

JUHUDI za kuzima vuguvugu la hasla linalompigia debe Naibu Rais Dkt William Ruto, zinaendelea kushika kasi kote nchini huku kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga akiendelea na shughuli zake bila wasiwasi.

Ijumaa, polisi katika Kaunti ya Kwale walitibua mkutano wa kisiasa ulioandaliwa na washirika wa Dkt Ruto katika uwanja wa maonyesho wa Ukunda.

Mkutano huo ulipokuwa ukivunjwa, Bw Odinga alikuwa akihudhuria mazishi Kaunti ya Kisii ambapo mkutano wa Dkt Ruto ulivunjwa Alhamisi.

Bw Odinga pia alikutana faraghani na viongozi wa eneo la Nyanza katika shule ya wasichana ya Nyamagwa.

Alipoondoka Kisii, Bw Odinga alielekea Kaunti ya Migori kuhudhuria mazishi.

Katika mikutano yake, Bw Odinga alikuwa akilindwa na maafisa wa usalama na kuandaliwa zulia jekundu.

Mkutano wa Kwale ulikuwa wa pili ulioandaliwa na washirika wa Dkt Ruto kutibuliwa ndani ya saa ishirini na nne.

Mnamo Alhamisi, polisi walisambatarisha mkutano ulioandaliwa na washirika wake Kaunti ya Nyamira.

Mkutano wa Ijumaa ulikuwa wa kumpigia debe mgombeaji huru katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, Bw Feisal Bader.

Dkt Ruto anamuunga Bw Bader katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Desemba 15 baada ya chama cha Jubilee kuamua kutokuwa na mgombezi.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na maseneta wa zamani Johnson Muthama, Hassan Omar na Dkt Boni Khalwale walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Wandani hao wa Ruto walikuwa wakutane na wafuasi wa Bw Bader katika hoteli ya Diani Reef kabla kufanya mkutano wa kisiasa katika uwanja wa maonyesho wa Ukunda.

Lakini polisi, wakiongozwa na kamanda wa kaunti dogo la Msambweni, Bw Nehemiah Bitok waliweka vizuizi katika barabara inayoelekea hoteli hiyo ya Diani Reef.

Baadaye, Bw Bitok na maafisa hao walielekea uwanja wa Ukunda na kuwafurusha wafuasi waliokusanyika wakisubiri kuhutubiwa na viongozi hao.

Hata hivyo, kamanda huyo wa polisi hakutoa sababu za kuzuia mkutano huo.

“Watu wanapaswa kurudi nyumbani sasa na mtaarifiwa na viongozi wenu sababu za kutoruhusu mkutano huo ufanyike,” akasema Bw Bitok.

Mnamo Jumatano, Baraza la Kitaifa la Ushauri wa Usalama (NSAC) lilitoa kanuni za kuandaa mikutano ya kisiasa zinazohitaji waandalizi kujulisha maafisa wa usalama siku tatu kabla ya tarehe ya mkutano.

Kanuni hizo zinazolenga kudhibiti mikutano ya hadhara kutokana na vurugu za kisiasa zilizoripotiwa hivi karibuni katika sehemu za nchi ziliidhinishwa na Baraza la Mawaziri Alhamisi.

Lakini katika ujumbe wake Facebook Bw Bader alidai kwamba maafisa wa polisi walitumiwa kuvuruga mkutano wao ambao ulilenga kuwaleta wagombeaji wengine wa kisiasa kumuunga mkono.

Bw Bader pia alidai kwamba, walinyimwa kibali kufanya mkutano kwa sababu hakukuwa na ilani ya siku tatu kwa vyombo vya usalama kabla kuandaa mkutano wa hadhara.

“Hatuwezi kupigana na polisi kwa sababu hatuna mabomu ya machozi au bunduki na mashini, sisi ni wananchi. Silaha zetu ni kura zetu. Tuna nguvu na dhamira ya kupigania kile ambacho ni haki yetu. Tutasonga mbele kwa ushujaa na bila shauku ili kushinda,” akasema.