Habari

Ruto azungumzia kufutwa kazi kwa Rashid Echesa

April 10th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Naibu Rais William Ruto amezungumzia suala la kufutwa kazi kwa Rashid Echesa ambaye alikuwa ni Waziri wa Michezo.

Akiongea kwenye mahojiano Jumanne na mwanahabari wa runinga ya Citizen Hussein Mohammed nyumbani kwake Karen, Ruto alisema kuwa Rais ana mamlaka ya kumfuta kazi jinsi alivyomteua.

“Rais hakutoa sababu yoyote iliyosababisha kumfuta kazi Bw Echesa sawa na namna ambavyo hakutoa sababu zilizomfanya kumteua katika baraza la mawaziri,” akasema Dkt Ruto.

Hussein: Waziri wa zamani Echesa amekuwa akitaka sababu iliyosababisha kufutwa kwake. Je, ni sababu gani ilisababisha kufutwa kwake?

Akijibu swali hilo, Ruto alitunga swali jingine.

“Hebu nikuulize mbona aliteuliwa? Ikiwa Rais hakutoa sababu ya kumteua hana wajibu wa kusema ni kwa nini alimfuta Echesa,” akasema Ruto.

Bw Hussein alijibu kwa kusema kwa kuwa Dkt Ruto ni mshirika katika asasi ya urais alikuwa katika nafasi nzuri kusema ni kwa nini Echesa alifutwa.

“Nadhani kuwa aliyemteua ana haki ya kumfuta kazi… Kwa kutoa sababu au kutotoa sababu,” akasema.

Farakano

Kabla ya kufutwa kwake, Bw Echesa alimzomea Bw Odinga akidai hana mamlaka ya kumfuta kazi kwa sababu siyo yeye alimwajiri. Bw Echesa ni mwandani wa Dkt Ruto.

Dkt Ruto alisema kuwa yeye hufuatilia kwa makini masuala yote ya uendeshwaji wa serikali.

“Mimi huwaita mawaziri na makatibu wa wizara kuwahoji kuhusu masuala yote ya serikali. Kama Naibu Rais, mimi hufuatilia miradi yote ya serikali inayotekelezwa,” akasema.

Hata hivyo, alifafanua kuwa asasi zote huru kama vile Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ziko huru na hazielekezwi na afisi ya rais.

“Nina imani katika utendakazi wa asasi zote za serikali. Nina haja kama Naibu Rais kufuatilia utendakazi wa DCI kuhusiana na uchunguzi kuhusu sakata za mabwawa ya Arror na Kimwarer,” Dkt Ruto akasema huku akisisitiza kuwa anaheshimu uhuru za asasi hiyo na zingine zinazochunguza ufisadi.

“Je, ni lini DCI amesema kwamba William Ruto amempigi simu au kwama ninaingilia uchunguzi? Sijasema uchunguzi huo sharti usimame. Kile nilisema ni kwamba uchunguzi huo usitumiwe kueneza uwongo kwamba Jubilee ni serikali fisadi,” akasema.