Jamvi La Siasa

Ruto hajakita mizizi kisawasawa serikalini – Joe Nyutu

January 4th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Joe Nyutu amedadisi kwamba shida nyingi za serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto zinatokana na idadi kubwa ya wafanyakazi wa umma kuegemea mirengo ya tawala za zamani.

“Serikali ya Rais Ruto iko na zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi ambao bado hawajaamini au kukubali kwamba yeye ndiye alishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, kwa kuwa walikuwa wameshawishika kuwa hangeibuka kuwa mshindi,” akasema seneta Nyutu.

Bw Nyutu alisema kwamba changamoto hiyo inapewa ugumu zaidi na baadhi ya wandani wake alioshinda uchaguzi nao kwa sababu “wamebaki butu kimaongezi, wamebweteka na ni watepetevu”.

“Wengine wao wana kasumba kwamba ni marais wadogo ambao wamegawana mamlaka ya urais,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba Rais Ruto yuko na changamoto kuu kwa kuwa ndani ya utumishi wa umma, ana maafisa wakuu ambao walikuwa watiifu kwa marais Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta huku yeye akiwa ndiyo anaanza kujipa mizizi ya kina.

“Haitakuwa rahisi kwa kuwa wengi ni wale ambao walikuwa wakijiandaa kupisha kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kuwa kiongozi wa taifa kwa mujibu wa harakati zilizokuwa zimesukwa na mtangulizi–Kenyatta–akitumia utumishi wa umma kumfungia nje Dkt Ruto,” akadai.

Seneta huyo aliongeza kwamba “kile kinachomsaidia Rais Ruto kwa sasa ni ngome zake kuu za kisiasa kubakia ngangari nyuma yake licha ya kuchochewa kwa kiwango kikuu wamuone kuwa muongo, chaguo la ovyo na ambaye hakufaa”.

Alisema kwamba busara ya Ruto kugawa serikali yake kwa ustadi mkuu ambapo viti kadha vyenye nguvu nyingi zilituzwa maeneo ambayo alipata kura chache pia kumesaidia kumweka ikulu akiwa na nafasi ya kutekeleza majukumu yake.

“Aidha, hatua ya Rais Ruto kuingia bungeni na akachumbia wajumbe wa ziada kuongeza idadi yake ya utiifu ilimfaa kumwezesha kusukuma mbele ajenda za manifesto yake kupita katika mabunge yote mawili,” akasema.

Katika msingi huo, Bw Nyutu alimtaka Mkuu wa Utumsihi wa Umma Felix Koskei kuhakikisha kwamba ameweka mikakati thabiti ndani ya taasisi zote zilizo chini yake ili kuzima usaliti na hujuma.

“Ni lazima utumishi wa umma uelewe kwamba utiifu huwa kwa serikali iliyoko mamlakani na ikiwa kuna yeyote anamkosa aliyekuwa akihudumu kabla ya Ruto kupanda, basi ajiuzulu aende akaajiriwe shambani mwake… Ni ukweli kwamba tuko na watu ndani ya serikali hii ambao wako katika njama ya kuhakisha Rais Ruto amekwama ndipo uongozi umtoke mwaka 2027,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba tetesi ambazo Rais yuko nazo dhidi ya mahakama ni za haki.

“Sote tunakubaliana kwamba katika kila gunia la viazi lazima kuwe na kiazi kimoja au viwili ambavyo vimeooza, hata ndani ya taasisi hii ya haki lazima kuwe nao wafisadi na walio ndani ya njama hiyo ya usaliti na hujuma,” akasema.

Seneta huyo alisema kwamba hali kwa sasa nchini ni kama ile ya abiria aliyekosa basi lake alipendalo kwa steji lakini akaabiri jingine na wakiwa katika safari, “anaomba lianguke kwa kuwa halikuwa chaguo lake”.

“Yeyote anayeombea Taifa la Kenya lisifaulu kwa msingi kwamba aliyeko mamlakani hakuwa chaguo lake, ni sawa na abiria anayeomba basi lianguke yeye akiwa ndani kwa sababu halipendi au hapendi dereva anayeliendesha,” akasema.

Aliwataja walio na mtazamo huo kama watu wasioona mbele na hata kufananisha hali hiyo na “washambuliaji wa kujitoa mhanga”.

[email protected]