Ruto: Hata Uhuru atafurahia enzi ya utawala wangu endapo nitachaguliwa Agosti 9

Ruto: Hata Uhuru atafurahia enzi ya utawala wangu endapo nitachaguliwa Agosti 9

NA SAMMY WAWERU

NAIBU Rais, William Ruto ambaye anamezea mate kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu Jumanne, Agosti 9 amemhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kwamba hapaswi kuwa na wasiwasi wowote kuhusu uongozi wake.

Dkt Ruto amemtaka Rais Kenyatta kuwa na imani, endapo atamrithi na kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya ataisukuma mbele na kuifanya kuwa bora.

Kauli ya Ruto ambaye anawania urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza, imeonekana kuwa jawabu kwa tashwishi ya Rais Kenyatta, ambaye amenukuliwa mara kadha akidai matamanio yake ni kuona atakayeibuka mshindi hana tamaa za ubinafsi.

Rais Kenyatta amesalia na chini ya siku mbili kukamilisha awamu yake ya pili na ya mwisho, na ametangaza kumuunga mkono kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance, Raila Odinga kumrithi.

Wawili hao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu baada ya kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018, kupitia mapatano ya Handisheki, hatua iliyoonekana kumghadhabisha Dkt Ruto.

Naibu Rais aidha amekuwa akilalamikia kutengwa katika maamuzi muhimu ya serikali ya Jubilee.

Jumamosi, Ruto alimtaka Rais kuondoa shauku yake ikiwa ataibuka mshindi.

“Rais Uhuru Kenyatta, ndugu yangu, tulishirikiana kufanya maendeleo kabla uhusiano wetu kutenganishwa 2018. Ningetaka kukuhakikishia, usiwe na wasiwasi na uongozi wangu. Jukumu letu kama viongozi ni kuhudumia Wakenya,” Ruto akasema, akizungumza katika mkutano wa Kenya Kwanza, Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.

Naibu wa Rais alitumia jukwaa hilo kusisitizia sera na ahadi zake kwa wananchi, kukomboa taifa endapo atambwaga mpinzani wake mkuu Bw Odinga.

“Na wewe ndugu yangu wa kitendawili (jina analotumia kumtania Raila Odinga kisiasa), ninakwambia Jumanne jioni kwa sababu nina imani nitakuonesha kivumbi nitakualika kikombe cha chai kisha nikupe majukumu yako kama kiongozi wa upinzani,” akasema.

Ruto hata hivyo alisema ikiwa ataibuka kidedea, hatafuata mkondo wa Rais Kenyatta kujumuisha kiongozi au viongozi wa upinzani kwenye serikali yake.

“Lakini namhakikishia yaliyofanyika miaka mitano iliyopita (akimaanisha Handisheki ya Machi 2018 kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga), ya kugawanya Wakenya sitafanya,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal wakomoa Crystal Palace katika mechi ya kwanza ya...

Liverpool wafungua kampeni za EPL 2022-23 kwa sare ya 2-2...

T L