Ruto hatarini kwa ‘kubagua’ vyama vidogo Mlima Kenya

Ruto hatarini kwa ‘kubagua’ vyama vidogo Mlima Kenya

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu kudumisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya ielekeapo Agosti, baada ya kuonekana kupuuza vyama vidogo vidogo kutoka eneo hilo kwenye ‘ndoa’ yake mpya vyama vya ANC na Ford-Kenya.

Imeibuka kuwa vyama hivyo havijatambuliwa rasmi kwenye muungano mpya wa Kenya Kwanza Alliance—unaovishirikisha vyama vya UDA (chake Ruto) ANC (chake Musalia Mudavadi) na Ford Kenya (chake Seneta Moses Wetang’ula).

Kwenye mkutano na wabunge wanaomuunga mkono katika makazi yake rasmi mtaani Karen, jijini Nairobi, Jumatatu, Dkt Ruto alifichua kwamba tayari washawasilisha usajili wa muungano huo kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa Dkt Ruto katika eneo hilo wameanza kutilia shaka nafasi yao kwenye muungano huo, wakishikilia kuwa vyama vyao vingepewa utambuzi tu kama vile ANC na Ford-Kenya, wanazoshikilia vinatoka katika eneo la Magharibi.

Baadhi ya vyama vidogo vidogo katika ukanda huo ni PNU, Usawa kwa Wote Party (chake Gavana Mwangi wa Iria wa Murang’a), TSP (chake mwanasiasa Mwangi Kiunjuri), Chama Cha Kazi (chake mbunge Moses Kuria-Gatundu Kusini), Tujibebe Wakenya Party (chake aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo), Narc-Kenya (chake mwanasiasa Martha Karua), Devolution Empowerment Party (chake Gavana Kiraitu Murungi wa Meru) kati ya vingine.

Baadhi ya vyama ambavyo vinaonyesha ama vimekuwa vikionyesha dalili za kuegemea mrengo wa Dkt Ruto ni TSP, CCK, Tujibebe Wakenya Party miongoni mwa vingine.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wanasema kuwa hatua ya vyama vyao kutotambuliwa kwenye muungano huo ni “dalili za hatari.”

“Kwa wakati wote ambao Dkt Ruto amekuwa akifanya kampeni zake katika eneo la Mlima Kenya, amekuwa akiwaahidi wenyeji kwamba watakuwa na usemi mkubwa katika serikali yake. Ikiwa huo ndio ukweli, mbona anavifungia nje baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa vikimuunga mkono? Ikiwa vyama hivyo ni vya kikabila, basi hata ANC na Ford-Kenya ni vya kikabila kwani asili yake ni eneo la Magharibi,” akasema mshirika mmoja wa Dkt Ruto, ambaye hakutaka kutajwa.

Washirika hao wanasema wanahofia huenda “wakafurushwa nje” kutoka UDA ikiwa hawatakuwa na “jukwaa” lao maalum kutetea maslahi yao.

“Kwa kawaida, chama huwa jukwaa la eneo fulani kutoa sauti yake kwenye muungano wa kisiasa. Hiyo ndiyo sababu ya uwepo wa vyama vya kimaeneo, hata ikiwa huwa vinafasiriwa kuwa vya kikabila. Ikiwa ‘ndoa’ ya Mlima na Dkt Ruto itaendelea, basi lazima atoe nafasi kwa vyama hivyo kushirikishwa kikamilifu kwenye muungano huo mpya,” akasema Bw Mwangi Kiunjuri, ambaye awali alikuwa mshirika wa Dkt Ruto.

Wadadisi wa siasa wanasema mwelekeo huo mpya unapaswa kumfungua macho Dkt Ruto, kwani huenda ahadi zake kwa wenyeji wa eneo hilo zikaanza kutiliwa shaka.

Wanasema ni hali ambayo inaweza kumrudisha nyuma sana kisiasa, ikiwa hataonyesha mapema kuwa atatetea na kulinda maslahi ya wenyeji.

“Kauli kuu ya wanasiasa ambao wamejitokeza pakubwa kutoka Mlima Kenya ni kigogo yeyote ambaye ataibuka mshindi kwenye uchaguzi wa Agosti kutilia maanani ufufuzi wa sekta ya kilimo,” akasema, kwani ndiyo kitegauchumi cha wenyeji.

Vile vile, wamekuwa wakisaka hakikisho la kujumuishwa ifaavyo kwenye serikali itakayobuniwa kutokana na idadi kubwa ya wapigakura.

Hivyo, lazima Dkt Ruto aanze kudhihirisha hilo mapema au awe kwenye hatari ya kupoteza uungwaji mkono ambao amejizolea kwa karibu miaka minne iliyopita,” asema Bw Felix Onyango, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Anaonya kuwa huenda hilo likawa kosa kubwa la kisiasa, ikizingatiwa kuwa tayari, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, amezindua rasmi kampeni zake katika eneo.

Baada ya mkutano mkubwa aliofanya kisiasa mjini Thika, Kaunti ya Kiambu, washirika wa Bw Odinga walitaja hilo kama “mwanzo wa harakati za kulikomboa eneo hilo kutoka mwa matapeli wa kisiasa.”

“Kama kuna nafasi, itamlazimu Dkt Ruto kuondoa dhana iliyopo miongoni mwa wenyeji, la sivyo atajutia uamuzi huo kwani huenda wakakosa kumuunga mkono,” akaeleza Bw Onyango.

You can share this post!

Cameroon wakomoa Gambia na kuingia nusu-fainali ya AFCON

JUNGU KUU: Hatua ya Mudavadi inaweza kumponza

T L