Bambika

Ruto: Huku nje Rachel ni mnyamavu lakini kwa boma ni kasuku

May 11th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa Kaunti ya Murang’a mnamo Ijumaa waliachwa wakiangua kicheko wakati Rais William Ruto alimtania hadharani Mama wa Taifa Rachel Ruto kwa madai kuwa ni mnyamavu nje lakini asiyependa masihara ndani ya boma.

Rais Ruto alikuwa ameandamana na Mama wa Taifa katika hafla ya upanzi wa miti katika eneobunge la Maragua na akampa nafasi ya kuhutubia wenyeji.

Wenyeji walimsifu Mke wa Rais wakimuita ‘mali safi’ kwa sauti na ndipo akachukua maikrofoni kuwahutubia.

Bi Ruto aliwasifu wenyeji kwa kujitokeza kwa wingi katika hafla hiyo na pia kuonyesha namna wanavyopenda kuhifadhi mazingira kupitia kukumbatia wito wa kupanda miti.

“Mungu awabariki na awatendee mema na ninawapenda,” Bi Ruto akamalizia hotuba yake iliyochukua chini ya dakika moja.

Mama wa Taifa Rachel Ruto akitoa hotuba fupi katika Kaunti ya Murang’a mnamo Mei 10, 2024. PICHA | MWANGI MUIRURI

Rais Ruto kando na kumsifu Mama wa Taifa kwamba ni mshirika wake wa kumsaidia mambo mengi na pia kumuombea, alizindua mchakato wa utani dhidi yake.

“Msihadaike vile ametoa hotuba ya maneno machache iwapotoshe kwamba yeye huwa hivyo nyumbani. Mambo kwa nyumba ni mengi… hayawi hivyo,” akasema Rais Ruto wenyeji wakiangua kicheko.

Ziara hiyo ya Rais Ruto ilimpeleka hadi kwa msitu wa Kawaharura ambapo aliongoza hafla ya kupanda miti 50,000 katika mpango wake wa kupanda miti 15 bilioni kabla ya 2032.

Aliandamana na viongozi wote wa Murang’a waliochaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.