Habari za Kitaifa

Ruto, Kalonzo watofautiana kuhusu polisi kutumwa nchini Haiti

March 24th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

SUALA linalozua mdahalo mkali kwa sasa nchini ni kuhusu ikiwa Kenya itapeleka polisi wake nchini Haiti au la.

Hili liliibuka baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo, Ariel Henry, kutangaza kujiuzulu mnamo Jumatatu.

Bw Henry alichukua hatua hiyo baada ya kupewa maonyo makali na kiongozi mkuu wa magenge ya uhalifu nchini humo, Jimmy ‘Barbeque’ Cherizier, kwamba lazima ang’atuke uongozini.

Makundi hayo yalikuwa yametishia kuanza maasi makali dhidi ya Bw Henry.

Licha ya mwelekeo huo, Rais William Ruto amekuwa akisisitiza kwamba lazima Kenya “iisaidie Haiti kurejea katika hali ya kawaida kiusalama”, hasa baada ya maeneo mengi kutekwa na magenge hayo ya uhalifu.

Hata hivyo, Rais Ruto amekosolewa vikali kwa msimamo wake, baadhi ya Wakenya wakisema serikali haikutathmini vilivyo suala la kutuma polisi Haiti. Wanateta nchi hiyo kuwa hatari kwani ingali imetwaliwa na magenge sugu.

Baadhi ya wale wamejitokeza kumkosoa Rais ni kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka.

Rais William Ruto alisema “Nimezungumza na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika, Anthony Blinken, na kumhakikishia kuwa Kenya haijabadilisha msimamo wake wa kuongoza kikosi cha polisi cha kimataifa kuisaidia Haiti kurejea katika hali ya kawaida. Tuko tayari kutuma kikosi hicho.”

Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka naye amemjibu, “Serikali hii ndiyo itawajibikia hali zozote zitakazowakumba polisi wetu, kwani wanatumwa nchini Haiti bila taratibu zifaazo kuzingatiwa. Bado tunapinga vikali uamuzi huu, ikizingatiwa kuwa asilimia 80 ya Haiti inadhibitiwa na magenge ya uhalifu.”