Makala

Ruto, Kibicho hawako pamoja Jubilee

July 11th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

NI mimba ambayo haifichiki tena ndani ya serikali ya Jubilee.

Naibu Rais William Ruto hasikizani kamwe na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho.

Kibicho, mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta, anasemwa kuwa anaaminika zaidi kiasi kwamba ndiye huteua wale watakaopewa kazi ya kulinda kiongozi wa nchi.

Amekuwa kwenye malumbano na Dkt Ruto katika kile baadhi ya wachanganuzi wanasema anatekeleza “mradi wa Rais.”

Aidha, Kibicho ni rafiki wa dhati kwa mratibu wa ratiba ya Rais Ikulu, Kinuthia Mbugua na ambaye hulaumu Dkt Ruto kama aliyechangia kuanguka kwake kupata awamu ya pili kama Gavana wa Nakuru katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Kiongozi mmoja serikalini mwenye ufahamu wa kinachoendelea Ikulu, anasema: “Ukicheza na Kibicho unacheza na Rais. Ni suala linalojulikana na wote ambao wanafanya kazi ndani ya serikali hii. Ndiye hutumiwa na Ikulu kusaka ukweli kuhusu hali yoyote na pale unampata Kibicho akiongea kuhusu sera za serikali, hisia za Rais ziko hapo.”

Anasema hataki kutajwa jina kwa sababu hili ni suala nyeti kabisa.

Katika hali hiyo, malumbano kati ya Dkt Ruto na Kibicho yanatafsiriwa ndani ya serikali kama Rais Kenyatta mwenyewe akimwandama Ruto akijaribu kumzima makali kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Ingawa Rais alimwahidi Ruto urithi wa Ikulu ifikapo mwaka 2022, mengi yamefanyika ambayo yanageuza ahadi hiyo kuwa nyingine tu ya kisiasa ambayo imepitwa na wakati. Kwa sasa, Rais Kenyatta anasaka urithi wa Ikulu ambao utaunganisha Wakenya wala sio jamii mbili kama ilivyofanyika katika chaguzi za 2013 na 2017,” anasema huyo mwandani ndani ya Ikulu akiongeza kuwa mradi huo umekabidhiwa Kibicho kuuratibu.

Na kwa kuwa naye Ruto yuko na wandani wake ndani ya Ikulu, inaripotiwa kuwa amepata dokezi kuhusu mradi huu wa Kibicho kwa niaba ya Ikulu na ndipo hali kati yao wawili imegeuka kuwa sawa na ile ya kujenga Mnara wa Babeli ambapo wote waliokuwa katika harakati hizo walipitanishwa lugha kiasi cha ujenzi huo kusambaratika.

Wiki jana, Kibicho alimteua aliyekuwa Kamishna wa Narok, George Natembeya, kuwa mratibu wa masuala ya usalama Rift Valley katika hali moja ya kuonyesha jinsi analenga kudhibiti Ruto katika ngome hii yake muhimu kisiasa.

Bw Natembeya anafahamika vyema kwa kuzima wandani wa Ruto mapema mwaka 2019 katika vita vya kutimua wakazi wasiokubalika katika Msitu wa Mau.

Katika majibizano yaliyozuka, Natembeya aliwasuta wandani hao kama vibarakala wa kisiasa wa Ruto na ambao hawangeshawishi vitengo vya kiusalama Narok kulegeza mikakati ya kuwatimua wote 40,000 ambao walikuwa katika msitu huo kinyume cha sheria.

Katika bunge la kitaifa, kiongozi wa walio wachache John Mbadi aliwasilisha hoja ya kumpongeza Natembeya kwa msimamo wake thabiti “dhidi ya ushawishi haramu wa Naibu Rais.”

Sasa, Natembeya amewajibishwa jukumu Rift Valley la kuweka usalama mikutano ya Ruto akiwa mashinani.

Mwishoni mwa Juni 2019 akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Kameme, Dkt Ruto aliulizwa kama alikuwa na habari kuwa ndani ya vitengo vya kudumisha usalama kulikuwa na maafisa ambao walikuwa wakimdharau.

Swali hilo lilijikita kwa msingi kwamba katika hafla kadhaa zake mashinani, kuna maafisa wa usalama ambao walikuwa wakimsusia hivyo basi kumwangazia kama aliyekuwa hatambuliwi na vitengo hivyo.

Kwa mafumbo, Ruto alijibu: “Mimi ni Naibu Rais wala sio mpikaji chai au askari rungu ndani ya serikali na ninajua jinsi nitalishughulikia suala hili.”

Wandani wa DP Ruto walikuwa wamemtambua Kibicho kama aliyekuwa akiwaelekeza maafisa hao wasusie hafla zake mashinani.