Ruto kona mbaya, onyo la Uhuru laonekana kumlenga

Ruto kona mbaya, onyo la Uhuru laonekana kumlenga

WYCLIFFE MUIA NA CHARLES WASONGA

HOTUBA za Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga wakati wa misa ya wafu ya mwendazake Stanley Matiba mjini Murang’a mnamo Alhamisi zimeibua hisia kali eneo la Bonde la Ufa huku wadadisi wakisema onyo la viongozi hao wawili kuhusu kampeni za 2022 lilielekezwa kwa Naibu Rais William Ruto.

Japo Rais Kenyatta hakumtaja naibu wake moja kwa moja, aliwataja na kuwaonya baadhi ya viongozi wanaoendelea kumpigia debe Bw Ruto kurithi urais 2022.

“Rais ameowaonya magavana Mwangi wa Iria (Murang’a), Mike Sonko (Nairobi) na Ferdinard Waititu (Kiambu) dhidi ya siasa za 2022 badala yake wanapaswa kuangazia utendakazi katika kaunti zao,” Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu alisema kupitia Twitter.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Prof Herman Manyora anasema Bw Ruto anapaswa kujiuliza iwapo muafaka kati ya Rais na Bw Odinga si kuhusu 2022, ni kuhusu nini.

“Uhuru na Raila wanaposema watu wanaopenda kung’aa kisiasa wakati wa machafuko, bila shaka hawarejelei (Aden) Duale au (Moses) Wetangula kwa sababu hao si watu wa kuwatisha. Ruto ndiye alilengwa na anapaswa kujipanga bila kuonekana kupinga muafaka,” anasema Prof Manyora.

Wakihutubu Alhamisi, Rais Kenyatta na Bw Odinga waliwapuuzilia mbali wandani wao wanaopinga muafaka huo wakisema unahusu amani na maendeleo nchini.

“Najua kuwa kuna watu ambao hawakufurahia niliposalimiana na ndugu yangu Raila. Baadhi yao wako upande wangu na wengine wako upande wake. Hata hivyo, ni shauri yao kwa sababu lengo letu ni kuleta amani nchini kwa manufaa ya Wakenya wote,” Rais Kenyatta.

Profesa Manyora anashikilia kuwa japo wawili hao walisisitiza kuwa muafaka wao hauna uhusiano wowote na siasa za 2022, siasa hizo za urithi zinafungamana na muafaka huo.

 

Ruto hatakikani 

Mchanganuzi huyo anasema kauli za Rais Kenyatta na Raila zinaonyesha wazi kuwa hawana imani ya Bw Ruto, akisema wanasaka mtu ambaye atalinda masilahi yao.

“Ni wazi wanataka atakaye mrithi rais 2022 awe mtu wa kuunganisha Wakenya ili muafaka wao hudumu..kwa maoni yangu, huyo mtu hawezi kuwa Ruto,”anaongeza Prof Manyora.

Hata hivyo, akihutubu mjini Nakuru jana, Bw Ruto alikanusha kuwepo na mgawanyiko katika chama cha Jubilee na kuwataka viongozi kufuata ushauri wa rais wa kukomesha siasa za 2022.

Wandani wa Bw Ruto sasa wanafasiri kauli ya Rais kwamba maafikiano yake na Raila hayahusu kinyang’anyiro cha urais 2022, na kwamba ataendelea kutekeleza masuala yaliyokubaliana, kama njama ya kumtenga Naibu Rais.

Hii ni kwa sababu Bw Odinga amebainisha wazi kuwa anataka Katiba ifanyiwe mageuzi ili kufanikisha utekelezaji wa baadhi ya masuala waliyokubaliana na Rais Kenyatta katika muafaka huo kama vile marekebisho katika mfumo wa uchaguzi na kuimarishwa kwa ugatuzi.

“Muafaka huo umesambaratika, wanataka refaranda na sisi hatutaki,” alisema kiongozi wa Wengi Bungeni, Aden Duale ambaye ni mwandani wa Bw Ruto.

 

Ruto anamkera Uhuru

Wadadisi wanasema tabia ya Bw Ruto kujibizana na Bw Odinga hadharani, haswa kuhusiana na pendekezo la kubadilisha katiba huenda inamkera sana Rais Kenyatta ambaye anamtarajia naibu wake kuchapa kazi badala ya kurushiana maneno na upinzani.

“Hisia za rais zilionyesha hasira zake dhidi ya wandani wake wanaoonekana kupinga muafaka kati yake na Raila,” alisema Profesa Edward Kisiang’ani.

Na Jumamosi, Bw Odinga akiwa Kajiado, alisema mabadiliko ya katiba ni lazima ili kulainisha utekelezaji wa ugatuzi nchini.

Viongozi wa ODM wamemshtumu Bw Ruto kwa kuhujumu muafaka kati ya rais na Bw Odinga wakisema mabadiliko ya katiba ni lazima.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alimshauri Bw Ruto kuunga mkono mabadiliko ya katiba iwapo angetaka kusalia serikalini baada ya uchaguzi wa 2022 .

“Ruto atakuwa kiongozi wa upinzani 2022 akiendelea kupinga mipango ya rais na Raila,”alisema Bw Malala.

Maelezo zaidi na Carolyne Agosa

You can share this post!

Ashangaza mpenzi kuchepuka bila haya akiiga mamake

MAKALA MAALUM: Abubakar, kakake Joho, ndiye Sultan kamili...

adminleo