Ruto kufukuzwa nyumbani

Ruto kufukuzwa nyumbani

Na WAANDISHI WETU

HUENDA Naibu Rais William Ruto akafurushwa kutoka makazi yake rasmi katika mtaa wa Karen, Nairobi, hivi karibuni, amesema Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP), Bw David Murathe.

Hivi majuzi, wandani wa Dkt Ruto walieleza wasiwasi wao kuhusu njama ya kumtimua Naibu Rais, huku baadhi yao wakidai kuna mpango wa kuteua waziri atakayetajwa kama ‘makamu wa rais’.

Bw Murathe alisema mipango hiyo “iko karibu kukamilika, na itawapata wengi kwa mshangao.”

Ingawa makazi hayo ndiyo rasmi ya Naibu Rais, Dkt Ruto amekuwa akiyatumia kufanya vikao na rubaa mbalimbali ambazo humtembelea kutoka maeneo tofauti ya nchi.

Dkt Ruto ameyapa makazi hayo msimbo wa Hustler’s Mansion, kauli inayofanana na jumbe ambazo amekuwa akitumia kuendesha kampeni zake.

Vikao hivyo vimekuwa vikionekana kama mikakati yake kujitayarisha kwa kinyang’anyiro cha urais cha 2022.

Alhamisi, Bw Murathe alisema juhudi za kumfurusha Dkt Ruto ziko karibu kukamilika kwani “hataruhusiwa kuendelea kuwatumbuiza waasi katika jahazi ambapo yeye ni nahodha mdogo tu.”

“Mikakati ya kumfurusha iko katika hatua za mwisho mwisho. Msiwe na tashwishi hata kidogo. Mtajionea,” akasema Bw Murathe, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Alhamisi usiku.

Kauli yake inajiri wakati uhusiano wa Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta umeendelea kudorora, hasa baada ya zaidi ya mabunge 40 ya kaunti kuupitisha mswada wa ripoti ya BBI.

Akiwa mshirika wa karibu wa Rais Kenyatta, matamshi ya Bw Murathe yamekuwa yakichukuliwa na wengi kwa uzito, kwani mara nyingi huwa yanatimia.

Mnamo 2016, Bw Murathe alitoa ‘utabiri’ kwamba Rais Kenyatta angebadilisha mwenendo wa utawala wake katika muhula wa pili, kwa kuwa mkakamavu na mkali zaidi, hasa dhidi ya watu wanaokumbwa na tuhuma za ufisadi.

Hayo yanaelezwa kutimia kwani mara tu baada ya kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, 2018, serikali ilianza juhudi kali za kuwakabili wafisadi.

Baadhi ya watu maarufu walijipata pabaya, miongoni mwao akiwemo aliyekuwa Waziri wa Fedha, Henry Rotich na aliyekuwa Katibu katika wizara hiyo, Dkt Kamau Thugge.

Bw Murathe pia ‘alitabiri’ kufurushwa kwa maseneta sita maalum ‘waasi’ katika Jubilee, Isaac Mwaura, Millicent Omanga, Mary Seneta, Victor Prengei, Naomi Waqo na Falhada Deqow.

Kiongozi huyo pia alisema Baraza la Kusimamia Chama (NMC) litakutana Jumatatu ijayo kuanza mchakato wa kumfurusha mbunge Caleb Kositany (Soy) kama Naibu Katibu Mkuu, kwa kuwafanyia kampeni wawaniaji wa chama cha UDA katika maeneobunge ya Matungu na Kabuchai.

Aidha, chama cha ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi kilitangaza mpango wa kumng’oa Dkt Ruto mamlakani. Mbunge Ayub Savula siku chache baadaye alisema kuwa amekusanya zaidi ya saini 126 za wabunge wanaounga mkono hoja ya kumng’oa Naibu Rais enzini.

Kwingineko, Dkt Ruto hatimaye amevunja kimya chake kuhusu marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) na kutangaza kuwa hataongoza mrengo wa kupinga mchakato huo. Tangu Jumanne wakati mabunge mengi ya kaunti yalipopitisha mswada wa marekebisho ya katiba, ikiwemo baadhi ya kaunti za ngome yake ya kisiasa, Dkt Ruto alikuwa ameepuka kuzungumzia suala hilo.

Lakini jana alipokuwa katika Kaunti ya Nandi, Naibu Rais alisema yuko tayari kukumbatia matokeo yoyote yatakayopitishwa na Wakenya wakati watakapopiga kura ya maamuzi. Kufikia sasa Kaunti ya Nandi na Baringo pekee ndizo zilizokataa kupitisha mswada huo.

“Kuna wengine wanatarajia eti mimi nitaongoza mrengo huu ama ule. Mimi ni mtu ambaye ninaamini katika demokrasia. Uamuzi utakaotolewa na Wakenya, mimi niko tayari kuunga. Kama ni katiba ya sasa ama ni katiba ambayo itakuja, mimi niko tayari,” akasema akiwa eneo la Kobujoi, eneobunge la Aldai, Nandi.

Dkt Ruto kwa muda mrefu amekuwa akipinga BBI pamoja na wandani wake wakisema ni uharibifu wa rasilimali za umma na muda ambao ungetumiwa kuletea wananchi maendeleo.

Lakini sasa baada ya madiwani wengi kutekwa na wimbi hilo linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, Naibu Rais anataka wanaoongoza mchakato mzima wasiache mtu yeyote nyuma ili nchi iwe na umoja.

“Lazima tukubali kuwa hatimaye mpango huu utaleta umoja wa nchi na kuwa kila mmoja wetu lazima akubali matokeo ya uamuzi wa Wakenya. Urekebishaji wa katiba haufai kufanywa kwa vitisho kwa sababu ni lazima kila mtu asikilizwe,” akasema. Hata hivyo, aliendelea kusisitiza kuwa jambo muhimu kuliko BBI ni kuboresha maisha ya Wakenya.

“Haya yote mwishowe kutakuwa na mkataba, na huo mkataba unaoandikwa saa hizi ni mkataba ambao unatueleza vile tutakavyogawanya mamlaka na pesa. Lakini ule mkataba muhimu zaidi ni mkataba ambao utatupa nafasi ya kuunda nafasi za kazi na biashara na mali,” akasema.

Ripoti ya Tom Matoke na Wanderi Kamau

You can share this post!

Liverpool hawatajishughulisha sana sokoni mwishoni mwa...

BI TAIFA FEBRUARI 27, 2021