Na CHARLES WASONGA
RAIS William Ruto mnamo Jumatatu, Januari 30, 2023, atafungua rasmi semina ya Bunge la Kitaifa na Muungano wa Mabunge ya Mataifa ya Jumuiya ya Madola (CPA).
Semina hiyo inalenga kuwahamasisha wabunge kuhusu haja ya wao kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika muhula huu wa Bunge la 13.
Semina hiyo ya siku nne inayofanyika katika mkahawa wa Pride Inn Beach Resort, kaunti ya Mombasa, inadhaminiwa na Bunge la Kitaifa na CPA.
Kulingana na taratibu za mabunge ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Madola, semina kama hiyo hufanyika mwanzoni wa kila muhula wa bunge.
“Hii semina inalenga kuwapa uwezo wanachama wa bunge la 13 katika nyanja zote za utendakazi bora wa bunge. Aidha, inalenga kuimarisha maadili ya kitaifa na misingi bora ya demokrasia ya bunge,” Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula akasema kwenye taarifa ya awali kwa wabunge kuhusu mkutano huo.
“Tumewaalika washirika wetu kutoka kituo cha kitaifa cha kuendeleza demokrasia Amerika (NDI) na Kituo cha Kitaifa cha Republican (IRI). Asasi hizi zitawezesha wabunge wetu kujifunza mengi kuhusu demokrasia ya mabunge mawili na utawala wa vyama vingi,” Bw Wetang’ula akasema.
Vile vile, inatarajiwa kuwa wabunge watafaidi kutokana na taratibu za kuendesha shughuli za bunge katika nchini zilizoendelea kama vila Uingereza na Amerika.
Mada zingine ambazo zitajadiliwa katika mkutano huo ni: wajibu wa muungano wa mabunge ya jumuiya ya madola (CPA); Kanuni ya Utangano wa Mamlaka na Majukumu, Taratibu za Bunge katika Mataifa ya Jumuiya ya Madola, Uongozi na Maadili hitajika kwa Wabunge.
Wabunge pia watahamasishwa kuhusu wajibu wa Bunge la Kitaifa katika mchakato wa Utayarishaji Bajeti, Wajibu wa Kamati za Bunge katika utekelezaji wa wajibu wa bunge wa kuhakiki Serikali Kuu, miongoni mwa masuala mengine yanayohusu bunge na wabunge.
Baada ya semina hiyo kufunguliwa na Rais Ruto, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi atatoa walisho kuhusu wajinu wa Afisi yake katika kushirikisha uhusiano kati ya Bunge na Serikali Kuu.
Kulingama na Agizo la Rais la 2023, Mkuu wa Mawaziri hushirikisha ajenda za kisheria za Wizara na Idara za Serikali Kuu na Bunge la Kitaifa kwa kushauriana na uongozi wa Kenya Kwanza katika Bunge la Kitaifa.