Ruto kuhudhuria sherehe za ushindi Msambweni leo

Ruto kuhudhuria sherehe za ushindi Msambweni leo

Na BRIAN OCHARO

NAIBU Rais William Ruto anatarajiwa kuzuru kaunti ya Kwale kuongoza sherehe za ushindi wa Mbunge wa Msambweni Feisal Bader, ambaye alimbwaga aliyekuwa mgombea wa ODM Bw Omar Boga katika uchaguzi mdogo wa majuzi.

Ziara hiyo itafanyika siku mbili tu baada ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kufanya mkutano na viongozi wa chama hicho kutathmini matokeo hayo yaliyoshtua wanachama wengi.

Katika mkutano wa ODM Jumanne uliofanywa faraghani, viongozi mbalimbali walidai kuwa ukosefu wa uratibu sahihi kati ya maafisa wa chama hicho ulichangia Bw Boga kushindwa katika kinyang’anyiro hicho.

Ilibainika pia mizozo kati ya maafisa wa chama hicho ilisababisha uhamasishaji duni wa wapigakura, ambayo ilipelekea idadi ndogo ya wapigakura katika maeneo ambayo yalizingatiwa kama ngome za Bw Boga kujitokeza uchaguzini.

Wakati wa mkutano huo ambapo waliohudhuria walinyang’anywa simu zao ili wasirekodi mazungumzo, ilisemekana ukosefu wa fedha pia uliathiri kampeni za chama hicho.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Bw Odinga alisema kuwa chama hicho sasa kinajiandaa kufanya kampeni za kupitisha BBI kwa maandalizi ya kura ya maamuzi.Wanachama wakiongozwa na Bw Odinga walijiliwaza kuwa, matokeo ya uchaguzi mdogo wa Msambweni yamekipa chama nafasi ya kujiangalia tena na kujipanga vizuri kwa siasa yanayosubiri chama hicho kutoka 2021 kwenda mbele.

Bw Odinga alisema kuwa mkutano huo ambao ulidumu kwa karibu nusu siku huko Diani, ulikipa chama fursa ya kupata picha wazi ya kile kilichoharibika na kusababishia mgombea wake kupoteza kiti hicho.

“Washiriki wetu wengi hapa wamepata nafasi ya kujieleza kwa uwazi ili tuweze kuzungumza kama familia na kufanya uamuzi. Wameweza kutambua masuala kadhaa ambayo yanahitaji kushughulikiwa,’ alibainisha Bw Odinga.

Chama hicho kimesisitiza kuwa bado ni maarufu kati ya wapigakura na kuonya wanasiasa wa Tangatanga kutotumia matokeo hayo kudharau umaarufu wa chama cha chungwa.

Viongozi wa chama hicho hata hivyo, walisema kuwa kupoteza kiti cha Msambweni haimaanishi kuwa chama cha chungwa kimepoteza umaarufu katika eneo la pwani.

Bw Odinga alisema kuwa matokeo ya uchaguzi huo ni moja ya mambo ‘mabaya’ ya 2020 ambayo chama hicho kinataka kuzika na kusahau kwani inaongeza nguvu na mikakati ya mashindano mengine makubwa yanayokuja.’

Hili (uchaguzi wa Msambweni) ni jambo ambalo liko nyuma yetu na tunasonga mbele kuelekea mwaka mpya,’ alibainisha.Kura ya maoni juu ya BBI na kampeni za 2022 ni masuala muhimu ambayo chama hicho kinasema kinataka kuzingatia licha ya janga la Covid-19 ambalo lilipunguza shughuli za kisiasa nchini mwaka huu.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho, ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM alisema chama hicho kilipoteza kura kwa sababu uchaguzi huo mdogo ulifanywa siku ya wiki wakati wapigakura wengi walikuwa katika maeneo yao ya kazi.

“Kwa hivyo ni mpumbavu tu ndiye atakayetumia hii kuamua kuwa umaarufu wa chama umepungua. Inawezekanaje? Ukisherehekea hiyo basi umepotea, ” akasema gavana huyo.

Kulingana na Bw Joho, mgombea wa ODM alipata kura za kutosha kwa kuzingatia idadi ndogo ya wapiga kura ambao walipata fursa ya kupiga kura.Kuenda mbele, Bw Joho amesema kuwa chama hicho kinatia nguvu tena na kitafanya kampeni za michubuko ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali.

Anabainisha kuwa chama hicho kinarudi kwa hali yake ya zamani kwa nia ya kuchukua kampeni hadi Uchaguzi Mkuu wa 2022. Bw Joho alibaini kuwa chama hicho kwa sasa kinachora mikakati ya siasa za 2022 na za BBI na kuwaonya wanasiasa wa Tangatanga kujiandaa kuona kivumbi ambayo yatathibitisha kuwa chama cha ODM bado kina nguvu na hakijapoteza mshiko katika sehemu yoyote ya nchi hii.

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed ambaye pia alihudhuria mkutano huo alisema kuwa ingawa chama kilipoteza kiti, ODM haiwezi kulinganishwa na Tangatanga, ambayo haina jina rasmi kama chama au vuguvugu.

“Tofauti kati ya ODM na Tangatanga ni kwamba ODM ni chama cha kisiasa ilhali Tangatanga haijulikani ni nini.Mara ya mwisho kusikia juu yao (Tangatanga) walikuwa katika Jubilee lakini waliacha chama kwa hivyo hatujui ni kitu gani , ‘alisema.

Bw Mohamed alidai kwamba DP ana wabunge chini ya 50 wanaoshirikiana naye katika Bunge la Kitaifa.“Wabunge 150 wako wapi? Ana Kimani Ichung’wa, Moses Kuria na Aisha Jumwa tu. Wako wapi wengine? Hatuwezi kutishiwa na uchaguzi mmoja tu. Sisi ni chama chenye wabunge wa kutosha, ”akasema Bw Mohamed.

Viongozi waliokuwa katika mkutano huo walimhakikishia Bw Odinga kwamba watakipigia depe chama hicho kuingoza umaarufu na kuhakikisha kuwa kinashinda viti kadhaa vya uchaguzi katika uchaguzi ujao.

You can share this post!

2020: Waliong’aa na kugusa Wakenya kwa njia ya kipekee

Wanafunzi wa wazazi wasio na karo wasifukuzwe shuleni...