Habari

Ruto kumkabili Raila Kwale

September 25th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

SIKU moja tu baada ya chama cha Jubilee kumzuia Naibu Rais William Ruto kumdhamini mwaniaji kwenye uchaguzi mdogo wa Msambweni, Kaunti ya Kwale, sasa amejitokeza kutangaza kuwa lazima apimane nguvu na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

Jana, Bw Ruto alikutana na Bw Feisal Bader ambaye atawania kama mgombea-huru na kutangaza kwamba atamuunga mkono.

Katika mtandao wake wa Twitter, Bw Ruto aliweka picha aliyopigwa akiwa na wabunge wa Pwani katika afisi yake ya Karen jijini Nairobi.

Wabunge hao ni pamoja na Mohammed Ali (Nyali), Athman Shariff (Lamu Mashariki), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), na Khatib Mwashetani (Lunga Lunga) ambao walikuwa wameandamana na Bw Bader.

Bw Ali aliweka picha hizo hizo na kueleza kuwa ‘watakuwa’ debeni kwenye uchaguzi huo.

“Msambweni iko sawa. Timu mgombea-wa-kujitegemea. Feisal Abdallah Bader. Acha watu waamue,” akasema Bw Ali kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook.

Sasa ni rasmi kuwa Bw Bader ambaye alikuwa msaidizi wa aliyekuwa mbunge wa Msambweni marehemu Suleiman Dori, atapambana na Bw Omar Boga ambaye kulingana na wadokezi atapata tikiti ya chama cha ODM.

Ikiwa wazi kuwa Bw Ruto atampigia debe Bw Bader baada ya mgombeaji mwengine, Bi Mariam Sharlet kukosa nafasi ya tiketi ya chama cha Jubilee, kutakuwa na siasa kali kati ya Naibu Rais na Bw Odinga.

Hali hiyo inatarajiwa kuwa sawia na ile iliyoshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa Kibra, Nairobi mwaka jana.

Kabla ya Bi Sharlet kutaka tiketi hiyo, alikuwa katika chama cha ODM lakini akajiuzulu na kutaka apewe tiketi ya Jubilee.

Kujiuzulu kwake kulifuatia kujiondoa kwa Waziri wa Fedha katika Kaunti ya Kwale, Bw Bakari Sebe, ambaye alikuwa anapigiwa upato na Gavana Salim Mvurya, ambaye wadokezi walieleza kuwa alikuwa anapata msukumo kutoka kwa Bw Ruto.

Kubadilika kwa mambo hayo kulijiri siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutembelea eneo la Kwale na kukutana na Bw Mvurya.

Hapo awali, Bw Bader ambaye ana uhusiana wa kiukoo na Bw Dori, alikuwa amepigiwa debe kupata tiketi ya chama cha ODM.

Mnamo Jumatano, Bw Odinga alikuwa ametoa shukrani zake kwa chama cha Jubilee kujiondoa kwenye kinyanga’anyiro hicho, licha ya Bw Ruto kusema alikuwa na maoni tofauti kuhusiana na hilo.

“Mimi nilikuwa na maoni tofauti kuhusiana na suala hili lakini tumekubaliana kama chama. Hata hivyo, ninasema kuwa mwaniaji yeyote ambaye anataka nimsaidie, basi aongee nami vizuri na nitatekeleza hilo,” akasema Bw Ruto baada ya kukutana na katibu wa chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju.

Bw Tuju alitangaza kuwa Jubilee haitadhamini mwaniaji kwenye uchaguzi huo kwa sababu ya ushirikiano wao wa amani na ODM.

Sasa ikiwa bayana kuwa Bw Ruto amepata nafasi ya kuingia kwenye siasa hizo za eneo la Msambweni, itasubiriwa kuonekana namna kivumbi kati yake na Bw Odinga kitakavyojitokeza wakati uchaguzi huo utakapokaribia.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Desemba 15 kama ilivyotangazwa na IEBC.