Ruto anamtaja naibu leo naye Raila ni kesho

Ruto anamtaja naibu leo naye Raila ni kesho

NA MOSES NYAMORI

MWANIAJI urais wa Muungano wa Kenya Kwanza, Dkt William Ruto, anatarajiwa kuteua mgombea mwenza wake hii leo Jumamosi.

Mpinzani wake Bw Raila Odinga wa Azimio la Umoja-One Kenya, pia anasubiriwa kumtangaza naibu wake kesho Jumapili.

Miongoni mwa wanaopigiwa upatu kuteuliwa na Dkt Ruto ni Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, Mbunge wa Kandara Alice Wahome na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru.

Utafiti wa kura ya maoni uliofadhiliwa na Nation Media Group ulionyesha kwamba kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi pia anapendelewa na Wakenya wengi (asilimia 19) kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto.

Hata hivyo, mkataba wa maelewano wa Kenya Kwanza unasema kuwa ni sharti mwaniaji wa urais na naibu wake watoke katika chama cha United Democratic Alliance (UDA), chake Dkt Ruto.

Katika upande wa Azimio, maafisa wa ngazi ya juu katika muungano walieleza Taifa Leo kuwa kuna uwezekano Bw Odinga akamtaja mgombea mwenza wake katika mkutano mkubwa wa kisiasa uwanjani Kamukunji; ambao ni sehemu kubwa ya historia za siasa zake.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imeweka makataa ya hadi Jumatatu kwa wawaniaji wa Urais kuwatangaza wagombeaji wenza wao.

Wakati wa mkutano huo wa kisiasa, Bw Odinga anatarajiwa kuyataja yaliyomo katika manifesto yake na pia kuwataja hadharani viongozi wakuu ambao watamvumisha kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mnamo Alhamisi, jopo lililokuwa likiwahoji wanaotaka kuwahi nafasi ya mgombeaji mwenza kwenye kambi ya Bw Odinga, lilimwasilishia majina matatu huku duru zikiarifu kinara wa Narc Kenya Martha Karua aliwapiku wenzake.

Wengine wanaoaminika kuwa kwenye orodha hiyo ni mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Jopo hilo lilikuwa linaongozwa na Waziri wa zamani na mwanasiasa mkongwe Noah Wekesa.

Mkuu wa bodi ya kampeni za Bw Odinga Ndiritu Muriithi ambaye pia ni gavana wa Laikipia, alieleza Taifa Leo kuwa Bw Odinga huenda akamtaja mgombeaji mwenza wake katika mkutano huo.

Bw Muriithi alisema mkutano huo wa kisiasa una umuhimu mkubwa kwa sababu utaashiria mwanzo rasmi wa kampeni za muungano huo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Tunasubiri kwa hamu mkutano huo kwa sababu utakuwa mkubwa na utaashiria tumeanza kampeni zetu. Vilevile tutakuwa tukiyafichua yaliyomo kwenye manifesto yetu na pia kuwatambua wanasiasa wakuu ambao watatekeleza jukumu muhimu kutuvumisha kote nchini,” akasema Bw Muriithi.

“Huenda akamtangaza mwaniaji mwenza wake ila hatujajadili. Kwa kuwa ameshapokezwa majina baada ya mahojiano kukamilika, inawezekana akatoa tangazo hilo,” akaongeza.

Naye mwandani wa Bw Odinga ambaye ni mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed alisema kuwa “Ni jambo linalowezekana, hatuwezi kupuuza chochote.”

Awali mkutano huo umekuwa umepangwa na muungano huo kutuliza joto la kisiasa katika Kaunti ya Nairobi hasa baada ya aliyekuwa Naibu Gavana wa Nairobi Polycarp Igathe kupokezwa tikiti ya kuwania ugavana.

Hatua hiyo iliwaghadhabisha wafuasi wengi wa mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi ambaye alionekana kuwa kifua mbele katika kiny’ang’anyiro cha kutwaa kiti hicho.

Naye Mkurugenzi wa Azimio la Umoja Raphael Tuju, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na Bw Wekesa waliashiria kuwa Bw Odinga atamtaja mwaniaji mwenza wake kesho Jumapili.

“Raila yupo huru kumtaja mwaniaji mwenza wake katika mkutano wowote wa kisiasa,” akasema Bw Tuju.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa 9 wa wizi wa mabavu watoroka seli za polisi Thika

TUSIJE TUKASAHAU: Ruto atueleze jinsi atakavyozima ufisadi...

T L