Habari za Kitaifa

Ruto kupaa tena nje ya nchi akiahidi kurejea na Sh160 bilioni

February 5th, 2024 2 min read

BENSON MATHEKA NA SHABAN MAKOKHA

RAIS William Ruto atafanya ziara yake ya 50 nje ya nchi kwa kuzuru Japan ambako anatarajia kupata Sh160 bilioni kufadhili miradi ya maendeleo ya serikali yake.

Dkt Ruto alitangaza kuwa atatua Japan kuanzia Jumanne hadi Jumatano kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Fumio Kishida aliyezuru Nairobi mwaka jana.

“Tunaenda Japan kwa sababu tuna mpango wa thamani ya Dola 1 bilioni (Sh160) bilioni, na Japan inatusaidia. Ni lazima tupange vyema,” alisema bila kutaja mpango huo.

Mkuu wa Mawaziri aliye pia waziri Wa Mashauri ya Kigeni na Wakenya wanaoishi ng’ambo, Bw Musalia Mudavadi aliondoka jana kwenda Japan kama sehemu ya rubaa ya Rais Ruto.

“Nitaondoka leo jioni (jana) na Rais ataungana nami baadaye baada ya kukutana na Rais wa Poland anayezuru Kenya,” Bw Mudavadi alisema akihutubu katika hafla ya maombi Kakamega ambayo Rais Ruto alihudhuria.

Rais Ruto alisema atajadili mradi wa Sh8 bilioni na Rais wa Poland.

“Leo nitakuwa mwenyeji wa Rais wa Poland Andrzej Sebastian Duda ambaye tuna mpango wa mradi wa Sh8 bilioni. Pesa hizi zitatumika kwa ustawishaji wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini Kenya,” alisema.

Hii itakuwa ziara ya 50 ya Dkt Ruto ugenini chini ya miaka miwili tangu aingie mamlakani. Wiki jana alizuru Italia kwa mkutano wa taifa hilo na mataifa ya Afrika ambayo ilijiri baada ya kuzuru Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Rais Ruto amekuwa akitetea ziara zake ugenini akisema zinasaidia kuwatafutia vijana kazi na kuimarisha uhusiano unaovutia uwekezaji wa moja kwa moja.

Tangu aingie mamlakani, Rais Ruto ametembelea zaidi ya nchi 40 za kigeni.

Hata hivyo, mrengo wa upinzani umekuwa ukimkosoa ukisema ziara hizo hazijasaidia kubadilisha hali ya uchumi Kenya ila zinafyonza pesa za mlipa-ushuru tu.

Bw Mudavadi alisema kuwa Japan imesaidia Kenya kwa kufadhili miradi ya afya, kilimo na elimu.

Mudavadi alisema Rais Ruto amepiga hatua kwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kote ulimwenguni na kurejesha sifa ya Kenya kwa nchi kama Amerika, Uingereza , China na Japan.

Alitetea ziara za Kiongozi wa Nchi na mawaziri na maafisa wa serikali yake ng’ambo akisema zinanuiwa kuimarisha uchumi wa Kenya.

“Ili tuweze kupigana na umaskini, Ruto lazima awaongoze ‘wanajeshi’ wake nje ya nchi na kutafuta marafiki wengine. Anaongoza Kenya kama nchi ya kwanza kuweka mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na mataifa 27 ya kigeni ili mazao yetu ya mashambani yafike soko la kimataifa,” akasema.

Alisema ziara za utawala wa Kenya Kwanza ughaibuni zinawezesha maendeleo ya kifedha ambayo ni muhimu kwa kupunguza matatizo ya madeni ya Kenya.

Aliwataka wanaokemea utawala wa Rais Ruto kukoma kukashifu safari za nje akisema zina manufaa mengi kwa nchi.