Habari

Ruto kusaidia familia ya mtoto aliyegongwa na msafara wake

June 8th, 2019 2 min read

Na GAITANO PESSA na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto ameahidi kusaidia familia ya mtoto aliyekufa baada ya kugongwa na gari lililokuwa kwenye msafara wake Ijumaa jioni mjini Busia.

Dkt Ruto alisema kwamba alizungumza na wazazi wa mtoto huyo Sidney Mambala Felix aliyekuwa na umri wa miaka saba na kuwapa rambirambi zake.

“Nimehuzunishwa na habari za kufariki kwa Sidney Mambala Felix, mvulana mdogo aliyekuwa na afya,” Dkt Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Ijumaa asubuhi.

Mtoto huyo aligongwa na gari la msafara wa Dkt Ruto alipokuwa akiondoka Budalang’i baada ya kuzindua mradi wa kupanda mchele.

“Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu hali ya mtoto huyo tangu nilipofahamishwa kisa hicho cha kusikitisha, na sasa, ninafariji familia ya Mzee Mzee Mambala, marafiki wake kwa kumpoteza mpendwa wao,” aliongeza Dkt Ruto.

“Nimezungumza na mzee kumpa rambirambi zangu na nikahakikishia familia msaada wangu wakati huu wa huzuni. Mungu alaze Mvulana mdogo Sydney mahali pema,” alisema Naibu Rais.

Wanahabari

Felix aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza alikanyagwa na gari la wanahabari wanaohudumu katika afisi ya Naibu Rais msafara ulipokuwa ukiondoka Butula ambapo alihutubia wazazi na wanafunzi wa shule za upili za Benedict’s Budalangi na Kingandole.

Ajali ilitokea dakika chache baada ya Dkt Ruto kuondoka kwa helikopta akiandamana na wabunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) na Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong.

Mtoto huyo alipelekwa kwanza katika hospitali ya Port Victoria kabla ya kuhamishiwa hospitali ya rufaa ya Busia alipokufa akitibiwa.

Walioshuhudia kisa hicho walisema kwamba baada ya kumgonga mvulana huyo walinzi wa Naibu Rais walimzuia msamaria mwema aliyetaka kumpeleka hospitali na badala yake wakamweka kando la barabara.

Walisema kwamba mtoto huyo alipata matatizo ya kupumua baada ya tukio hilo.

Wazazi wake walimpeleka Port Victoria Hospital akiwa katika hali mahtuti, Rosemary Adem aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema alikuwa katika hali mbaya. Polisi katika kituo cha Port Victoria walisema ajali hiyo iliripotiwa katika kituo chao na wanaendelea na uchunguzi. Mnamo Ijumaa usiku, Dkt Ruto alisema alikuwa amefahamishwa na kwamba angehakikisha mtoto huyo angepata matibabu.