Ruto kuteua mwaniaji mwenza bila kushauri viongozi wa UDA

Ruto kuteua mwaniaji mwenza bila kushauri viongozi wa UDA

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu wa Rais William Ruto, kimempa mwaniaji wake wa urais mamlaka ya kuteua mwaniaji mwenza bila kushauriana na viongozi wa chama hicho.

Baada ya kutengwa katika chama cha Jubilee, Naibu wa Rais amenukuliwa mara kadhaa akisema kwamba atatumia UDA kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Iwapo Dkt Ruto atapeperusha bendera ya chama cha UDA, ataruhusiwa kuteua mwaniaji mwenza anayetaka bila kushauriana na viongozi wakuu wa chama au Kamati Kuu (NEC).“Mwaniaji wa urais ataruhusiwa kuteua mwaniaji mwenza anayemtaka,” inasema Katiba ya chama cha UDA.

Katiba ya UDA pia imemruhusu Dkt Ruto kuendelea kuhudumu kama Naibu wa Rais hadi Mei, mwaka ujao bila kumtaka kujiuzulu mapema kutoka chama cha Jubilee.

Tofauti na ODM ambacho kinahitaji mwaniaji wa urais kuwa mwanachama wa kudumu miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu, chama cha UDA kimesalia kimya kuhusu muda ambao mwaniaji anastahili kuwa mwanachama kabla ya kuruhusiwa kuwania urais.

“Mwaniaji wa urais ni sharti awe mwanachama na awe amelipa ada iliyowekwa. Vilevile, mwaniaji wa urais anafaa kuungwa mkono na angalau wanachama 1,000 kutoka Kaunti zisizopungua 24 kote nchini,” inasema Katiba.

Mwaniaji wa urais, hata hivyo, ni sharti aidhinishwe na NEC na iwapo wagombea wa urais zaidi ya mmoja watajitosa, atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura za wajumbe ndiye atapeperusha bendera ya chama.

Naibu wa Rais Ruto angali katika njiapanda kuhusu mwaniaji mwenza wake katika uchaguzi mkuu ujao.Wanasiasa wa Tangatanga kutoka eneo la Mlima Kenya wamekuwa wakishinikiza Dkt Ruto kuteua mwaniaji mwenza wake kutoka ukanda huo.

Wanaopigiwa upatu kuwa wawaniaji wenza wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya ni wabunge Gachagua Rigathi (Mathira), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ichung’wah (Kikuyu) na aliyekuwa waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

Hata hivyo, wanasiasa wa Tangatanga kutoka maeneo mengine ya nchi kama vile Pwani na Magharibi pia wameshikilia kuwa mmoja wao ni sharti awe mwaniaji mwenza.

Lakini Dkt Ruto atakuwa na kibarua kigumu zaidi iwapo kiongozi wa ODM Raila Odinga ataachana na Rais Uhuru Kenyatta na kuamua kushirikiana na Naibu wa Rais.Bw Odinga itabidi awe mwaniaji mwenza wa Ruto – hatua ambayo huenda ikasababisha wanasiasa wa Tangatanga wa eneo la Mlima Kenya kugura UDA.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wansema kuwa ushindi wa mwaniaji wa UDA katika Wadi ya Rurii, Kaunti ya Nyandarua, wiki mbili zilizopita, ni ithibati tosha kwamba Dkt Ruto ana uungwaji mkono mkubwa katika eneo la Mlima Kenya.

You can share this post!

Rufaa ya BBI kung’oa nanga juma lijalo

Wito serikali itoe sodo bila malipo