Habari za Kitaifa

Ruto kutia saini Mswada wa Fedha 2024 wakati wowote sasa baada ya wabunge 195 kupitisha


WAKATI wowote kuanzia sasa Rais William Ruto anatarajiwa kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024 kuwa sheria kuiwezesha serikali kukusanya Sh347 bilioni kufadhili bajeti ya mwaka wa 2024/2025.

Hii ni baada ya wabunge 195 kupiga kura ya NDIO kuunga mkono mswada huo ulivyofanyiwa marekebisho huku wabunge 106 wakiupinga.

Wabunge wote 304 waliokuwa ukumbini walishiriki katika upigaji kura ilha kura za wabunge watatu ziliharibiwa na hivyo kukosa kuzingatiwa.

“Matokeo ya upigaji kura kwa Mswada wa Fedha wa 2024 ulivyofanyiwa marekebisho ni kama yafuatavyo: Upande wa Ndio kura 195, upande wa LA kura 106, kura zilizoharibiwa ni tatu na hakuna aliyesusia upigaji kura,” Spika Moses Wetang’ula akatangaza baada ya shughuli ya upigaji kura kukamilika.

Baadaye, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha Kuria Kimani aliitwa kufunga mjadala kuhusu mswada huo na akaungwa mkono na naibu mwenyekiti wa Kamati hiyo Mbunge wa Ainamoi Benjamin Lang’ata.