Ruto kutua Kisii kuzima ushawishi wa Matiang’i

Ruto kutua Kisii kuzima ushawishi wa Matiang’i

Na Ruth Mbula

NAIBU Rais William Ruto amepangiwa kuzuru Kisii kwa siku tatu katika juhudi za kuzima umaarufu wa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangí kabla ya Uchaguzi Mkuu 2022.

Ingawa Dkt Matiang’I hajatangaza azma yake ya kugombea urais, inachukuliwa kwamba wawili hao wanapimana nguvu wakilenga kura zaidi ya milioni moja za eneo hilo.

Naibu Rais alikuwa amepanga kuzuru eneo hilo mapema lakini masharti ya Covid -19 yanayopiga marufuku mikutano ya kisiasa yakasitisha mipango yake.Amepanga sasa kuzuru Kaunti hiyo hii leo, Jumapili na Jumatatu.

Hata hivyo, amekuwa na mikutano kadhaa katika makao yake Karen, Nairobi, na wanasiasa kutoka eneo la Gusii tangu mwanzo wa mwaka huu.

Ziara ya Dkt Ruto imejiri siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi wanaomuunga mkono Bw Matiangi kutangaza kuwa watakuwa na chama chao.

Safari yake hasa imechochewa na ripoti kuwa baadhi ya viongozi ikiwemo waliomo katika kambi yake, wanapigia debe kuundwa kwa chama imara cha eneo hilo kitakachotetea maslahi ya jamii hiyo.

Na Wanaoshabikia chama cha eneo hilo wanaamini kuwa ni njia moja ya kuileta pamoja jamii hiyo. Huku akikabiliwa na uhalisia kuwa huenda anapoteza eneo hilo, Naibu Rais alikusanya haraka washirika wake kutoka eneo hilo na kuandaa ziara hiyo.

Viongozi wanaomuunga mkono walisema wazo la jamii hiyo la kuwa na chama cha kieneo ni tishio kwa vyama vikubwa.

“Hatua hii bila shaka itaumiza uungwaji mkono wa vyama vingine. Tulijitahidi kufanya United Democratic Alliance ing’ae eneo la Kisii lakini juhudi hizi huenda zikaambulia patupu ikiwa hatutaungana kukomesha tisho linalotukabili,” alisema Mbunge kutoka Kisii ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

You can share this post!

Ushawishi wa Kalonzo Pwani wafifia 2022 ikinukia

Mbunge ataka wapewe uhuru kubadilisha hoja za Rais katika...