Ruto kuzuru USA, Uingereza siku 12

Ruto kuzuru USA, Uingereza siku 12

Na KITAVI MUTUA

NAIBU Rais, William Ruto anatarajiwa kusafiri hadi Amerika na Uingereza kuanzia Jumapili hii ambapo atakutana na viongozi wa nchi hizo na pia Wakenya wanaoishi katika mataifa hayo mawili.

Kutokana na ziara hiyo ambayo itachukua siku 12, Naibu Rais hatashiriki kampeni kali ya kujivumisha huku duru zikiarifu ataandamana na Kinara wa ANC Musalia Mudavadi pamoja na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara) na Rigathi Gachagua (Mathira) kati ya wasaidizi wake na wandani wake wengine.

Hii itakuwa ziara ya kwanza ya Naibu Rais Amerika tangu achaguliwe kama Naibu Rais mnamo 2013.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika lisilo la kiserikali la Carnegie Africa Program lenye makao yake Washington DC, Naibu Rais anatarajiwa kuhutubu katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Georgetown, Jumatano Machi 2.

Mkutano huo utajadili maendeleo, ustawi wa kiuchumi na uongozi bora katika mataifa ya Afrika Mashariki na bara zima la Afrika chini ya mwenyekiti Karen Bass, ambaye ni mwanachama wa Bunge la Amerika.

Bi Bass pia ni mwenyekiti wa kamati ndogo ya Masuala ya Kigeni kuhusu Afrika, Haki za Kibinadam na Afya katika Bunge la Congress.

“Tuna furaha kuwa tutakuwa mwenyeji wa Naibu Rais wa Kenya Dkt William Ruto na mwanachama wa Bunge la Congress Karen Bass kuzungumzia siasa na sera,” ikasema taarifa fupi katika mtandao wa shirika hilo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Georgetown ambaye ana uraia wa Kenya na Amerika Ken Opalo ataongoza kikao hicho pamoja na Zainab Usman ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Amani Barani Afrika Carnegie.

Naibu Rais anatarajiwa kuzungumzia sera ya Kenya kuhusu vita dhidi ya ugaidi, mataifa ya kigeni pamoja na mpango wake wa ufanisi wa kibiashara iwapo atafanikiwa kushinda Urais mnamo Agosti.

Ziara hiyo inakuja ikiwa imesalia miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa mnamo Agosti 9.

You can share this post!

Messi, Ronaldo au Morata kusimamia harusi Dybala, Gabriela

Wimbo waelezea hisia za Uhuru akiachana na Ruto

T L