Habari Mseto

Ruto mbioni kutafuta uungwaji mkono Kisii

October 31st, 2019 1 min read

Na JOSIAH ODANGA

NAIBU Rais William Ruto yuko mbioni kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa katika eneo la Kisii kutokana na ziara nyingi ambazo amekuwa akifanya katika eneo hilo.

Tangu Mei 2019 Dkt Ruto amezuru eneo hilo karibu mara tano, ambapo amekuwa akiongoza hafla za kuchangisha fedha kusaidia makanisa, shule, wahudumu wa bodaboda na makundi ya wanawake.

Isitoshe, amezindua miradi ya ujenzi wa barabara, taasisi za kiufundi na kuongoza hafla za kufuzu kwa mahafala katika taasisi mbalimbali za elimu.

Kutokana na ziara hizo, Ruto anaonekana kuimarisha ufahamu wake kuhusu mahitaji ya wakazi na eneo hilo kwa ujumla.

Katika hotuba zake, amekuwa akiyatatamka maneno ya Ekegusii kwa urahisi bila usaidizi wowote.

Katika ziara yake aliyofanya majuzi alitembelea maeneo ya Ekerenyo, Tente katika eneobunge la Mugirango Kaskazini. Vile vile, alizuru maeneobunge ya Mugirango Magharibi na Kitutu Masaba, ambapo aliwashangaza wakazi kutokana na ufahamu wake mkubwa wa lugha ya Kikisii na namna alivyoyataja maeneo hayo bila ugumu wowote. Maeneo hayo yamo katika Kaunti ya Nyamira.

“Tunaweka lami barabara ya Kijauri-Nyansiongo-Metamaywa; Metamaywa-Mosebeti; Mosebeti-Kebirigo,” akaeleza bila kusoma popote.

Wanufaika

Vilevile, aliyataja majina ya wakazi ambao walinufaika na mpango wa usambazaji stima.

“Bi Subano Alosi ambaye ni mkazi katika eneo la Tente, Bw Alfred Makori Nyangweso kutoka eneo la Ekerenyo na Bi Grace Kemunto kutoka kijiji cha Gekano wamenufaika na stima,” akaeleza.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema ni dhahiri kuwa Dkt Ruto amefanikiwa kuingiana na wakazi kila anapozuru eneo hilo.

Hata hivyo, wanasema kuwa mbinu hiyo itampa kura, ila si kiasi kikubwa.

“Familia ambazo amezitembelea zitaendelea kumkumbuka na kumuunga mkono. Hata hivyo, huenda mbinu hiyo isimfae kwani ni vigumu kumfikia kila mtu kwa njia hiyo,” anasema Bw Omondo Okumu ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.