HabariSiasa

Ruto na Mudavadi wakwaruzana tena

January 4th, 2019 2 min read

DAVID MWERE Na BENSON MATHEKA

VITA vya maneno kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi, viliongezeka Alhamisi huku Mudavadi akimtaka Ruto kukoma kutumia mali ya umma kununua wanasiasa wamuunge mkono.

Bw Mudavadi alipuuzilia mbali ujumbe wa viongozi kutoka Kaunti za Bungoma na Busia waliomtembelea Bw Ruto nyumbani kwake Sugoi akiwataja kama washirika wake waliozoea kutangatanga naye ili wapate pesa.

“Naibu Rais anafaa kuacha kutumia mali ya umma kualika watu kwake kwa lengo la kutusi na kushambulia viongozi wengine anaochukulia kimakosa kuwa washindani wake. Kuna hekima katika kujenga daraja za urafiki kuliko kuchoma moja uliyo nayo,” Bw Mudavadi alisema kwenye taarifa iliyotiwa sahihi na msemaji wake Kibisu Kabatesi.

Akihutubia viongozi wa Bungoma na Busia mnamo Jumatano nyumbani kwake Sugoi, Bw Ruto aliwalaumu wanasiasa wanaotaka kumzuia kupata tiketi ya chama cha Jubilee bila rekodi ya maendeleo kwa Wakenya.

Bila kutaja majina, Bw Ruto alisema haogopi ushindani lakini akawaonya watu hao kwamba haitakuwa mteremko kuidhinishwa kuwa wagombea urais bila rekodi yoyote ya maendeleo.

Mwishoni mwa mwaka 2018, Bw Mudavadi alimwalika mwenyekiti wa Jubilee David Murathe kaunti ya Vihiga ambapo alitoa matamshi yaliyochoma washirika wa Ruto kwamba Naibu Rais anafaa kustaafu pamoja na Rais Kenyatta.

Alhamisi, Bw Mudavadi alisema Bw Ruto hafai kuogopa wapinzani wengine hata kabla ya kupata tiketi ya Jubilee. “Mara ya mwisho tulisikia kwamba Jubilee haina mgombeaji urais kwenye uchaguzi wa 2022. Kwa hivyo, Naibu Rais anafaa kukabiliana na mahasimu wake katika Jubilee badala ya kushutumu kila mtu kiholela,” alisema.

Kulingana na Bw Mudavadi, Bw Ruto hafai kulaumu viongozi wa upinzani kwa kukosa kutekeleza miradi ya maendeleo na akamtaka amsaidie Rais Kenyatta kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo ikiwa anataka rekodi ya kutumia akipata tiketi ya Jubilee.

“Tabia ya Naibu Rais kutangatanga kila mahali inaonyesha wazi ishara za kufadhaika, kuogopa na kuchoka. Katika hali hii, Naibu Rais anatumia mbinu zote chafu, ikiwa ni pamoja na vitisho kumlazimisha mkubwa wake, Rais Kenyatta kumtangaza kuwa mrithi wake,” alisema Bw Mudavadi.

Kiongozi huyo wa chama cha ANC alimtaka Bw Ruto kufuata ushauri wa Rais Kenyatta kuacha kampeni za mapema na kuzingatia maendeleo ya nchi.

“Ruto ni Naibu Rais wa Kenya. Kiapo chake ni uaminifu kwa Wakenya, Jamhuri na Rais wa Kenya. Sawa na Rais, anafaa kuwa nembo ya umoja wa nchi. Kutangatanga Kenya akitusi Wakenya wengine ni kuacha majukumu yake ya kutelekeza uaminifu na kiapo cha kutumikia Jamhuri ya Kenya,” alisema Bw Mudavadi.

Naye Katibu wa chama cha Kanu Nick Salat pia alimshambulia Bw Ruto kwa kualika jumbe za wanasiasa kwake ili kutusi viongozi wengine.