Michezo

Ruto na Raila matumaini tele Harambee Stars itajinyanyua

June 25th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

LICHA ya kupoteza mechi ya kwanza baada ya kichapo cha 2-0 mikononi mwa Algeria, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga anaamini kwamba kikosi cha Harambee Stars kina uwezo wa kufanya vyema katika mechi mbili za Kundi C zilizobaki.

“Baada ya kukaa nje kwa kipindi cha miaka 15, kwa mara nyingine tulishuhudia vijana wetu wakijikakamua licha ya matokeo ambayo wengi hawakuyatarajia. Mlijitahidi vilivyo, lakini kuteleza si kuanguka. Taifa zima liko nyuma yenu. HarambeeStars tunawatakia kila la heri kwenye mechi zilizosalia katika ratiba ya AFCON 2019,” alisema Raila Odinga.

Naibu Rais, William Ruto naye alisema: “Nilijiunga na wananchi uwanjani Camp Toyoyo mtaani Jericho usiku kushuhudia vijana wetu wakikabiliana na Algeria. Ingwa tulishindwa, naamini tuna kikosi imara kinachoweza kufanya vizuri katika mechi ijayo dhidi ya Tanzania. Ikiwa tutacheza jinsi tulivyocheza katika kipindi cha pili, bila shaka tutaandikisha matokeo mema katika mechi mbili zilizobaki za AFCON.”

Aliyekuwa katibu wa tawi la Nairobi la FKF, Micheal Esakwa alisema Harambee Stars ilikosa wachezaji wazoefu katika mechi hiyo.

Stars walifungwa bao la kwanza dakika ya 34 kutokana na mkwaju wa penlti kupitia kwa Baghdad Bounedjah baada ya Dennis Odhiambo kumchezea ngware Youcef Atal katika eneo la hatari.

Bao la pili lilipatikana kupitia kwa Riyad Mahrez wa klabu ya Manchester City ambaye kombora lake lilimchanganya beki wa kushoto Aboud Omar kabla ya kujaa wavuni.

“Kwa hakika tilikosa wachezaji wa uzoefu kama Allan Wanga, Jese Were na David Ochieng Cheche ambao wangakabiliana vyema na wapinzani hao. Baadhi yao waliogopa kwa vile hawajazoea mechi kubwa za kimataifa,” alisema Esakwa

“Baada ya kufungwa bao la pili nilishuhudia baadhi ya wachezaji wetu wakipoteza matumaini, hali iliyowapa wapinzani nafasi kubwa ya kutawala uwanjani kwa kipindi kirefu, lakini tulipoanza kucheza vizuri, muda ulikuwa umeyoyoma.”

Mechi ya mataifa jirani

Stars watarejea uwanjani dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania Alhamisi kwa mechi ya pili kabla ya kuvaana na Senegal katika mechi ya mwisho kundini.

“Senegal ni timu inayoongoza barani Afrika kwenye viwango bora vya FIFA kutokana na ufanisi wake kupitia kwa mastaa wake akiwemo Sadio Mane wa Liverpool, lakini pia sisi tuna Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur,” alisema shabiki Paul Mbote wa Kibera.

“Si wakati wa kumshutumu kocha kwani wakati umefika na sasa tunafaa kumuunga mkono tukiamini atafanya vyema katika mashindano hayo,” aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Kibera Black Stars.

“Kutokana na jinsi walivyocheza katika kipindi cha pili dhidi ya Algeria pamoja na zile za kupimana nguvu dhidi ya Madagascar na baadaye DR Congo, huenda vijana wetu watashangaza wengi nchini Misri,” aliongeza shabiki mwingine Rose Imbuye.