Ruto na Raila wazidi kuraruana kuhusu utawala wa Jubilee

Ruto na Raila wazidi kuraruana kuhusu utawala wa Jubilee

Na WAANDISHI WETU

NAIBU Rais William Ruto, jana alimkosoa Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa matamshi yake kwamba serikali ya Jubilee imeshindwa kufanikisha ahadi ilizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katika hotuba zake za hivi majuzi, Bw Odinga amekuwa akimkejeli Dkt Ruto kwa kutoa ufadhili wa vifaa kama vile wilbaro kwa wananchi, ilhali serikali anayosimamia ilikuwa imeahidi makuu wakati wa kampeni.

“Yale yote yalikuwa ni porojo. Sasa wamerudi kueneza porojo tena. Wakenya wameerevuka,” Bw Odinga alisisitiza jana, alipokuwa kanisani mtaani Soweto, Kaunti ya Nairobi.

Lakini akizungumzia suala hilo, Naibu Rais alidai ODM ina njama ya kuvunja handisheki ili kujitakasa isihusishwe na changamoto ambazo zimekumba utawala wa Jubilee kufikia sasa.Akizungumza kanisani eneo la Londiani, Dkt Ruto alidai ni Bw Odinga aliyesababisha mkanganyiko serikalini alipoibuka na mchakato wa kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Tunajua njama yenu. Mko na njama ya kuondoka lakini mnataka kutuachia vurugu. Mlituambia BBI ndiyo itasaidia kuleta mabadiliko kwa hivyo tunawasubiri mmalize hiyo,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Odinga alipuuza wanaodai kwamba Rais Kenyatta hayuko makini kwa handisheki akisema ana hakika kiongozi wa nchi hawezi kumcheza shere.Alisema kwamba handisheki yake na Rais Kenyatta ilitokana na mazungumzo ya dhati kati yao na wanaosema kwamba atasalitiwa wanadanganya.

“Tulikaa, tukazungumza kwa muda mrefu kabla ya kusalimiana na Uhuru na hawezi kumsaliti Raila. Tulikuwa wawili, wale ambao walikula kiapo cha urais. Wanaotoa kauli kama hizo ni takataka,” alisema Bw Odinga.

Mnamo Jumamosi, Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, alinukuliwa akisema iwapo Jubilee haiko tayari kuadhibu wanaopinga BBI, ODM kiko tayari kuchukua nafasi yake ya upinzani.

Bw Odinga aliwaambia vijana kwamba BBI ina mengi ya kuwafaidi na anachofanya Dkt Ruto ni kuwapotosha ili waikatae wasinufaike.

Kwingineko, Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama cha KANU, ambaye pia ni Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi, ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuharakisha uthibitishaji, uhakikishaji na upasishaji wa sahihi zinazounga mkono mswada wa BBI.

Akihutubia umma katika kisiwa cha Faza, Kaunti ya Lamu Jumamosi, Bw Moi aidha aliwasuta wanasiasa hapa nchini kwa kutomheshimu Rais Uhuru Kenyatta.

“Rais Kenyatta ndiye yuko mamlakani hadi Agosti, 2022. Lazima tumpe heshima yake na Mungu akichagua mwingine ifikapo 2022, pia tuna wajibu wa kuendelea kumheshimu,” akasema Bw Moi.

Mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket ambaye alikuwa ameandamana na Bw Moi kwenye ziara yake Lamu, alimsuta Dkt Ruto kwa kuendeleza kampeni za kupinga BBI na handisheki.

“Ni unafiki wa namna gani ikiwa mkubwa wako ameanzisha jambo unalofahamu vyema kwamba ni la kumfaidi mwananchi ilhali wewe unazunguka hapa na pale kupinga. Je, mikokoteni italeta chakula kwa meza?” akauliza Bw Kamket.

Mbunge Mwakilishi wa Kike Lamu, Bi Ruweida Obbo kwa upande wake alishikilia kuwa wakazi wa Lamu wanaunga mkono BBI kwani ni suluhu ya kipekee itakayohakikisha kabila zote zinafaidi uongozi nchini.

Ripoti za Benson Matheka, Valentine Obara na Kalume Kazungu

You can share this post!

Kiini cha wavulana kutorejea shuleni

Kipute cha Kenya Cup charatibiwa upya mchujo ukinukia