Habari

RUTO: Ninafuata mkondo wa uongozi wa mdosi wangu Rais Kenyatta

August 28th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais William Ruto amesema kwa sasa anafanya kazi kulingana na maelekezo ya Rais Uhuru Kenyatta.

Dkt Ruto amesema majukumu anayofanya kama Naibu wa Rais anayatekeleza kwa mujibu wa maagizo ya Rais.

“Sina wizara yoyote ninayoongoza, hivyo basi niko katika nafasi kumsaidia bosi wangu kufanya kazi. Tumekubaliana na Rais staili anayotaka ndiyo tutafuata,” akasema Naibu wa Rais.

Rais Kenyatta (TNA) na Bw Ruto (URP) walichaguliwa 2013 kama Rais na Naibu Rais mtawalia, kisha baadaye wakavunja vyama vyao na kuunda chama kikubwa cha Jubilee (JP) kilicholeta pamoja takriban vyama 12 vya kisiasa.

Dkt Ruto anasema awamu ya kwanza ya serikali ya Jubilee alikuwa na majukumu mengi, yanayojumuisha uzinduzi wa miradi ya ujenzi wa barabara, stima, ufunguzi wa taasisi mbalimbali za kiufundi, kati ya mingine.

“Awamu ya pili Rais alionelea afanye kazi kwa njia tofauti. Vile Rais anavyotaka, ndivyo tutafanya. Nitafanya majukumu anayopendekeza, tayari nimefanya aliyonipa,” akaelezea.

Naibu wa Rais alisema hayo Alhamisi usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, na ambapo alikiri kuna msukosuko ndani ya JP.

Mgawanyiko wa chama hicho tawala ulianza kushuhudiwa baada ya Machi 2018, kufuatia salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye kwa sasa anashirikiana kwa karibu na serikali.

Salamu hizo maarufu kama Handisheki, zilipelekea kuibuka kwa makundi mawili; ‘Kieleweke’ unaoegemea upande wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, na ‘Tangatanga’ upande wa Naibu Rais.

Makundi hayo yanaendelea kutofautiana kisiasa, lile la Tangatanga likihisi Handisheki inalenga kuzima ndoto za Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Ni kufuatia salamu za heri kati ya Rais Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga tume ya maridhiano ndiyo BBI ilibuniwa, ambapo ripoti yake inapendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho.

Hata hivyo, kulingana na Dkt Ruto nia yake na Rais ni kuhakikisha azma ya Jubilee imetekelezwa. Rais ameonekana kutegemea Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali Dkt Fred Matiang’i kutekeleza sera zake.