Habari za Kitaifa

Ruto: Ningetumia Kenya Airways kwenda Amerika ingekuwa ghali zaidi

May 26th, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

RAIS William Ruto ametetea matumizi ya ndege ya kibinafsi kwa ziara yake ya Kiserikali nchini Amerika iliyokamilika Ijumaa, akisema kwamba ilimgharimu kiasi cha chini ikilinganishwa na iwapo angetumia ndege za shirika la kitaifa nchini, Kenya Airways (KQ).

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X (awali Twitter), Jumapili, Rais anaonekana kujibu shutuma na malalamishi kwamba alitumia gharama isiyopungua Sh200 milioni kukodisha ndege ya kibinafsi ya kifahari kwa ziara hiyo.

Nimesikia malalamishi kuhusu mbinu ya usafiri niliyotumia kwenda Amerika. Mimi kama mdhibiti mzuri wa matumizi ninayeongoza kwa mfano bora, naweza kusema kiasi nilichotumia ni kidogo kuliko kile KQ ingelipisha,” akasema Dkt Ruto.

Ni ujumbe ulioibua hisia nyingi, wengi wakiuliza iwapo alimaanisha kwamba Wakenya wakwepe kutumia shirika hilo la kitaifa kwa safari za ndege. Baadhi pia walionekana kutosadiki iwapo ni ghali zaidi kutumia usafiri wa umma kuliko ule wa kibinafsi.