Ruto, Raila kumenyania kiongozi wa wengi bungeni

Ruto, Raila kumenyania kiongozi wa wengi bungeni

NA DAVID MWERE

MVUTANO mkali unatazamiwa hii leo Jumanne Bungeni kati ya kambi ya Rais William Ruto ya Kenya Kwanza na Azimio ya Raila Odinga kuhusu kiongozi wa wengi huku pande zote mbili zikidai wadhifa huo.

Wadhifa huo unaong’ang’aniwa na mirengo hiyo miwili mikuu nchini tayari umevutia Spika wa Bunge Moses Wetang’ula wa Kenya Kwanza anayetazamiwa kuamua ni upande upi ni wa wengi na upi ni wa wachache.

Shughuli ya kwanza ya kikao chake cha kwanza kuandaliwa tangu hotuba ya Rais iliyofanyika Alhamisi wiki iliyopita itakuwa kuunda kamati ya Biashara za Bunge (HBC), inayopanga na kupatia kipaumbele biashara inayofanyika Bungeni.

Katika Bunge la Seneti, suala hilo tayari limetatuliwa kwa sababu Kenya Kwanza ndicho chama chenye idadi kubwa huku kikiwa na maseneta 36 ikilinganishwa na 30 wa Azimio na mmoja kama mwaniaji huru.

Mbunge wa Belgut, Nelson Koech, alisema Spika ataamua ni nani atakayekuwa kiongozi wa wengi Bungeni ambaye moja kwa moja atakuwa mwanachama wa HBC.

“Hili ni suala ambalo bila shaka litahitaji mwongozo kutoka kwa Spika. Linapaswa kutatuliwa kabla ya kusonga mbele,” alisema Bw Koech.

Haya yanajiri wakati Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah (Kenya Kwanza) na mwenzake wa Ugunja, Opiyo Wandayi (Azimio) wanadai kila mmoja kushikilia wadhifa huo wa kiongozi wa wengi.

“Spika atahitajika kutoa uamuzi wake wa kina kuhusu ni nani ambaye ni kiongozi wa wengi leo,” alisema Bw Ichung’wah.

“Lakini kwa maoni yangu, mimi ndiye kiongozi wa wengi kwa sababu ya idadi ya wabunge ambao Kenya Kwanza inao Bungeni,” alihoji Mbunge wa Kikuyu.

Hata hivyo, Bw Wandayi alisisitiza kuwa ndiye kiongozi wa wengi na hakuna kinachohitajika kutatuliwa na Spika kwa sababu sheria “inasema wazi.”

“Hakuna cha kuamua hapa. Si wajibu wa Spika kuamua ni wapi kiongozi wa wengi na wa wachache wanapaswa kutoka,” alisema Bw Wandayi.

“Wanaomtaka Spika kutoa uamuzi kuhusu suala hili wanapaswa kuacha kupoteza muda wao. Wanapaswa kusoma katiba, Sheria kuhusu Vyama vya Kisiasa na Kanuni za Bunge,” alihoji mbunge wa Ugunja.

Akihutubia mkutano wa Kundi la Wabunge wa Kenya Kwanza Naivasha, Rais Ruto alisema muungano wake ndio wenye idadi kubwa Bungeni.

“Tusijidanganye. Tuna idadi na sisi ndio wengi katika Bunge la Taifa. Hakuna vinginevyo,” alisema Rais.

Kifungu 108 cha Katiba kinatambua afisi za kiongozi wa wengi na kiongozi wa wachache katika Bunge. Aidha, kinaeleza kuwa kiongozi wa wengi atakuwa mtu anayeongoza Bungeni chama au muungano wenye idadi kubwa naye kiongozi wa wachache ni kiongozi katika Bunge wa chama au muungano wa pili kwa idadi.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyibiashara walia kukosa biashara kituo cha mizigo cha...

Mulembe imani tele Mudavadi atawakwamua

T L