Ruto, Raila sasa waibiana ahadi

Ruto, Raila sasa waibiana ahadi

NA WANDERI KAMAU

BAADA ya Naibu Rais William Ruto na mwaniaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, kuzindua manifesto zao tayari kwa uchaguzi wa Agosti 9, imebainika kuwa wawili hao wanakopana kwa ahadi wanazotoa kwa Wakenya.

Wawili hao wamekita manifesto zao katika sekta tano kuu ambazo ni; Kilimo, Afya, Elimu, Viwanda na Uchumi kwa jumla.

Kwenye manifesto aliyozindua Alhamisi eneo la Kasarani, Nairobi, Dkt Ruto aliahidi kufanya kila juhudi kuimarisha sekta ya kilimo, ikizingatiwa kuwa ndiyo inayotegemewa na mamilioni ya Wakenya kujiendeleza kimapato.

Baadhi ya mikakati aliyotangaza kuiboresha ni kutenga Sh8.8 bilioni kufufua sekta ya ufugaji.

Alisema fedha hizo zitaelekezwa kwenye mikakati ya kuwasaidia wafugaji wa mifugo ya maziwa kuwasaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini.

Vilevile, aliahidi kutoa mitaji kwa wakulima hao kupitia vyama vya ushirika ili kuwasaidia kuboresha kilimo chao. Alitoa ahadi ya kuboresha kilimo cha mpunga, kahawa na majanichai.Kwenye manifesto yake, Bw Odinga pia alitangaza mikakati kama hiyo. Baadhi ya ahadi alizotoa ni kuwasaidia wakulima kupata mikopo ya kuendeleza kilimo chao, kuimarisha matumizi ya teknolojia kwenye kilimo, kuendeleza utafiti, kubuni bima ya mifugo kati ya mengine.

Kuhusu elimu, huku Bw Odinga akiahidi masomo ya bure kutoka chekechea hadi chuo kikuu na kuajiri walimu wote waliofuzu ambao hawajaajiriwa, Dkt Ruto ametaja kuwaajiri zaidi ya walimu 100,000 katika kipindi cha miaka miwili katika utawala wake. Naibu Rais pia analenga kuimarisha mfumo wa elimu mbali na kulainisha shughuli za kutoa ufadhili na mikopo kwa wanafunzi.

Kuhusu ufufuzi wa uchumi, suala la ufufuzi wa biashara ndogo ndogo, linaonekana kulingana. Dkt Ruto aliahidi kutenga Sh50 bilioni kila mwaka kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kujiendeleza kupitia vyama vya ushirika. Kijumla, mpango huo ni sehemu ya Hazina ya Hustler (tabaka la chini), aliosema kwamba utatengewa jumla ya Sh250 bilioni kati ya mwaka 2022 na 2027, ikiwa ataibuka mshindi. Pia, alitangaza mkakati wa kutambua rasmi biashara hizo.

Kwa upande wake, Bw Odinga aliahidi kutoa vyeti vya kuzitambua biashara hizo za juakali, sawa na Dkt Ruto. Pia, aliahidi kutoa mikopo midogo midogo kwa wafanyabiashara hao kupitia vyama vya ushirika, kutathmini mfumo wa utozaji ushuru, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kubuni mfumo wa kutoa mafunzo kwao.

Kuhusu afya, Dkt Ruto aliahidi kufadhili hospitali zote za umma, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata matibabu bila malipo yoyote. Pia, amehidi kubuni mpango ambao utalazimishaa kila Mkenya kuwa na kadi ya Bima ya Kitaifa ya Hospitali (NHIF) ili kumsaidia kupata matibabu katika hospitali za kibinafsi na umma bila matatizo yoyote. Sawa na Dkt Ruto, Bw Odinga ameahidi kutoa afya bora na yenye malipo ya chini kwa wote. Pia, ameahidi kubuni Hazina Maalum ya Matibabu ya Dharura, sawa na mpango wa NHIF.

Katika kuboresha uchumi, sanaa na matumizi ya mitandao, wawili hao pia wanaonekana kutoa ahadi sawa. Kwa upande wake, Dkt Ruto ameahidi kuweka mikakati kuhakikisha kuwa kila makazi nchini yanapata huduma za mtandao wa intaneti. Ameahidi kujenga nyaya za kusambaza intaneti zenye umbali wa kilomita 100,000. Nyaya hizo zitasambazwa katika maeneo tofauti kama shule katika kaunti zote 47. Bw Odinga naye ameahidi kubuni vituo maalum vya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) kote nchini, ambavyo vitakuwa vikitumika na Wakenya kwa huduma za mtandao wa intaneti. Pia ameahidi kusambaza intaneti katika shule na taasisi nyingine kote nchini.

Kuhusu ujenzi wa nyumba, wawili hao wameeleza mikakati sawa ya kuboresha sekta hiyo. Dkt Ruto ameahidi kuhakikisha sekta hiyo inabuni zaidi ya nafasi 100,000 za ajira kwa vijana ambao watakuwa wakimaliza mafunzo yao kutoka Vyuo vya Kiufundi (TVETs), kwa kujiinga katika sekta ya ujenzi. Ameahidi pia kuongeza idadi ya nyumba zinazojengwa nchini kutoka 50,000 hadi 250,000 kwa mwaka, ili kuwawezesha Wakenya wa mapato ya chini kumiliki nyumba. Kwa upande wake, Bw Odinga ameahidi kushirikiana na kaunti kuisaidia serikali ya kitaifa kujenga nyumba zaidi ili kuwawezesha Wakenya wa mapato ya chini kumiliki nyumba. Pia ameahidi kubuni mazingira bora kwa mashirika ya ujenzi ili kuyawezesha kujenga nyumba nyingi zaidi ambazo baadaye zitauziwa Wakenya kwa bei rahisi.

UFISADI

Ijapokuwa kwa kiwango kikubwa ahadi za vigogo hao zinafanana, Dkt Ruto analaumiwa kwa kutoeleza mikakati ambayo atachukua kuhakikisha amekabiliana na suala la ufisadi.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema mfanano huo wa manifesto unaashiria kuwa hakuna jambo jipya ambalo raia wanafaa kutarajia kutoka kwa serikali ijayo.

“Kwa tathmini ya kina, hizo ndizo ahadi zilizotolewa na miungano ya kisiasa ya hapo awali kama vile NASA, Jubilee na Cord kwenye chaguzi kuu za mwaka 2013 na 2017,” asema Bw Tony Watima, mtaalamu wa masuala ya kichumi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Hatima ya kandanda iko mikononi mwa rais mpya...

WANDERI KAMAU: Adhabu kali dhidi ya msanii Kelly onyo kwa...

T L