Ruto, Raila wakoroga chama cha Kingi PAA

Ruto, Raila wakoroga chama cha Kingi PAA

MAUREEN ONGALA na ALEX KALAMA

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi, Bw Amason Kingi, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuamua mwelekeo ambao chama chake kipya cha Pamoja African Alliance (PAA), kitachukua kuhusu uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Baadhi ya wanasiasa wanaounga chama hicho wameashiria watampigia debe Naibu Rais William Ruto kwa urais, huku wengine wakisema watasimama na kinara wa ODM Raila Odinga.Kwa upande wake, Bw Kingi hajabainisha wazi mwelekeo watakaochukua, lakini mapema mwaka huu, alikutana na viongozi wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) mjini Mombasa ambapo alisema walijadili uwezekano wao kushirikiana kisiasa.

Mmoja wa viongozi wanaoegemea PAA ambao wameonyesha nia ya kumuunga mkono Dkt Ruto ni Diwani wa Wadi ya Shimo la Tewa, Bw Sammy Ndago ambaye ni mmoja wa wandani wa Bw Kingi.Bw Ndago, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Kilifi, aliibua maswali hivi majuzi alipokutana na Dkt Ruto mjini Nairobi.

Katika mahojiano na Taifa Leo, diwani huyo anayemezea mate kiti cha ubunge cha Kilifi Kusini mwaka ujao, alisema PAA iko tayari kumuunga mkono mgombea urais yeyote atakayetimiza matakwa ya Wapwani.’PAA ni kama mwanamke anayetongozwa na tutamfuata yule atakayekuja na mazuri.

Tutamuunga mkono Ruto ama Raila, bora awe atashughulikia matakwa yetu vilivyo. Ni lazima mgombeaji urais afuate mkataba tutakaoweka pamoja,’ akasema.Mkutano wake na Dkt Ruto ulitokea siku chache baada ya kubainika kuwa, kuna baadhi ya wafuasi wa PAA ambao wanataka kumuunga mkono Bw Odinga kwa urais.Wakati Bw Odinga alizuru Pwani hivi majuzi, duru zilisema baadhi ya wanasiasa wanaojihusisha na PAA walikuwa wamepangiwa kutangaza wazi msimamo wao wa kutaka kuungana na waziri huyo mkuu wa zamani, hata kama hawatakuwa ndani ya ODM.

Mipango hiyo ilitibuka dakika za mwisho kwa sababu zisizojulikana, huku Mwenyekiti wa ODM tawi la Kilifi, Bw Teddy Mwambire, akisema ajenda hiyo itatekelezwa wakati mwingine.Licha ya mipango hiyo kutibuka, Seneta Maalumu aliyeteuliwa kupitia Chama cha Jubilee, Bi Christine Zawadi, alisimama kutangaza uamuzi wake wa kumuunga mkono Bw Odinga kwa urais ila yeye mwenyewe atawania kiti cha Mwakilishi wa Wanawake Bungeni kupitia kwa PAA mwaka ujao.

‘Mimi ni seneta wa Jubilee lakini wewe ni Rais wangu. Nitalijaza kapu lako la urais ila kupitia kwa Chama cha PAA,” akasema, katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Bw Odinga Malindi.Bw Kingi alitoa wito wa umoja baina ya viongozi wa Pwani ili waungane kutatua changamoto zinazokumba wakazi wa ukanda huo tangu jadi.

Akihutubu Jumanne katika mkutano wa vijana na viongozi wanaotaka kuwania viti kupitia PAA mwaka ujao, alisema tofauti miongoni mwao ndizo huleta vizingiti katika kutatua matatizo ya Wapwani.“Kutofautiana kwa sisi viongozi wa kisiasa hapa Pwani ndio kumechangia jamii zetu kuzidi kutaabika.

Jameni hebu na tuache ubinafsi na tuangalie yale matatizo yanayowakumba watu wetu ili tuone ni jinsi gani tunaweza kuyatatua,’ alisema Bw Kingi.Aliahidi kuwa PAA itajitolea kutatua changamoto kama vile kufifia kwa uchumi, migogoro ya ardhi miongoni mwa nyingine kwa manufaa ya wananchi.

Ilibainika kuwa, viongozi na wanachama waliohudhuria mkutano huo walishauriana pia kuhusu uwezekano wa kuanzisha mazungumzo ili waungane na vyama vingine vilivyo na mizizi Pwani kuunda muungano mmoja. Katika mahojiano na Taifa Leo jana, Bw Mwambire alisema ODM ina nafasi nzuri sasa kushinda urais mwaka ujao na itakuwa bora kama Wapwani wataungana na chama hicho.

‘Itakuwa bora iwapo vyama vya Pwani vitakuwa na mazungumzo ya jinsi tunaweza kufanya kazi pamoja. Itakuwa si vyema iwapo tutaonekana kujitenga wakati huu,’ akasema.

You can share this post!

Cotu yamtaka Matiang’i asikize kilio cha polisi

Samaki waoza kwa ukosefu wa jokofu la hifadhi

T L