LEONARD ONYANGO: Ruto, Raila watumie mitandao ya kijamii kusema na vijana

LEONARD ONYANGO: Ruto, Raila watumie mitandao ya kijamii kusema na vijana

Na LEONARD ONYANGO

BAADA ya kuwania urais mara tano bila mafanikio, kiongozi mpya wa Zambia Rais Hakainde Hichilema aliamua kubadili mbinu yake ya kusaka kura.

Mbinu yake mpya ilikuwa kukumbatia vijana – na wadadisi wanaamini kwamba ushindi wake wa kishindo aliopata katika uchaguzi mkuu wa Agosti, mwaka huu, ulitokana na kura nyingi alizopigiwa na vijana.

Hichilema, 59, ni miongoni mwa matajiri wakubwa katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati japo alizaliwa katika familia maskini.Alipowania urais kwa mara ya kwanza mnamo 2006, wadadisi wa masuala ya siasa nchini humo wanasema, kuwa ilikuwa vigumu kwa bwanyenye Hichilema kutangamana na raia wa kawaida pamoja na vijana.

Lakini baadaye, Hichilema alibadili mbinu akawa mnyenyekevu na akatumia mitandao ya kijamii kama vile Twitter na Facebook kutangamana na vijana.Hichilema alitumia mitandao ya kijamii kujibu maswali ya vijana na hata kuahidi kuwapa baadhi yao kandarasi ya kuoka keki siku yake ya kuapishwa.

Alitumia mitandao ya kijamii kuelezea ahadi na maoni yake kwa vijana na raia wote wa Zambia.Hata baada ya kushinda urais miezi miwili iliyopita Rais Hichilema angali anatumia mitandao ya kijamii kuwahakikishia vijana kwamba serikali yake inashughulikia changamoto zao.

Japo kinara wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakikutana na makundi ya vijana kujipigia debe, hawajafanya mengi kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia vijana – ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya wapigakura nchini.

Bw Odinga na Bw Ruto wamekuwa wakitumia mitandao kuonyesha mikutano yao mbashara katika maeneo wanayozuru. Kila wanapokutana na vijana, wanachapisha kwenye kurasa zao za Facebook na Twitter maandishi ya kijilugha cha sheng’. Kulingana na wanasiasa, kila kijana wa chini ya umri wa miaka 35 anazungumza ‘sheng’ – jambo ambalo si kweli.

Bw Odinga na Dkt Ruto – ambao wanapigia upatu kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, hawajakuwa wakitumia mitandao ya kijamiikujibu maswali ya vijana. Badala yake, vijana wamekuwa wakitumia mitandao ya viongozi hao kurushiana cheche za matusi.

Ni jambo la kusikitisha kwamba idadi kubwa ya wanasiasa wa humu nchini wamekodisha ‘mamluki’ wa mtandaoni, maarufu kama wanablogu, ambao hutumia mitandao ya kijamii kuchafulia majina wapinzani wao kwa kueneza propaganda.Mitandao ya kijamii inafaa kutumiwa na wanasiasa kama chombo cha wanasiasa kutangamana moja kwa moja na wapigakura vijana na wala si kuitumia kuchafuliwa wapinzani wao sifa.

You can share this post!

Mali ya Sirma hatarini kuuzwa na madalali

WANDERI KAMAU: Tuchunge ndimi zetu tunapoelekea 2022

T L