Ruto: Rais hatakuwa ameafikia ajenda zake atakapostaafu

Ruto: Rais hatakuwa ameafikia ajenda zake atakapostaafu

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais, William Ruto amedai Rais Uhuru Kenyatta hataweza kuafikia ajenda zake atakapostaafu 2022.

Baada ya kuchaguliwa kuhudumu awamu ya pili na ya mwisho 2017, Rais Kenyatta alisema analenga kufanikisha na kuimarisha afya bora na nafuu kwa wote, usalama wa chakula, makao bora na ya bei nafuu na sekta ya viwanda, chini ya Ajenda Nne Kuu, kabla kuondoka madarakani.

Kulingana na Naibu Rais, mipango na mikakati hiyo ilisambaratishwa na maridhiano kati ya Rais na kinara wa ODM, Raila Odinga, mnamo Machi 2018 maarufu kama Handisheki.

Wawili hao wamekuwa wakishirikiana sako kwa bako, licha ya Bw Raila kuwa kiongozi wa upinzani nchini.Ni hatua ambayo imeashiria kusababisha Dkt Ruto kutengwa katika serikali anayoshiriki kuongoza. Akiendeleza kampeni zake eneo la Shamata, Nyandarua, Ijumaa kusaka kura kumrithi Rais Kenyatta mwaka ujao, Ruto aliahidi kuendeleza ajenda alizoasisi kiongozi wa nchi.

“Mimi nasema hivi vile tulikuwa tumekubaliana, hata kama Rais wetu anaenda kustaafu si mimi nipo? Tutaweka Sh100 bilioni kuboresha viwanda, uongezaji thamani na kuimarisha sekta ya biashara,” Naibu Rais akasema. Akifufua safari ya uhusiano wake na Rais Kenyatta kati ya 2013 na 2017, Ruto alisema alisimama kidete na kiongozi wa nchi licha ya ushindi wao wa Agosti 8 kuharamishwa na mahakama ya juu zaidi.

Ushindi wa Rais na naibu wake ulifutiliwa mbali na jopo la majaji wa mahakama hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu, David Maraga, ambaye kwa sasa ni mstaafu, kwa kile walihoji ulikumbwa na udanganyifu.Kiongozi wa ODM, Bw Raila chini ya muungano wa Nasa, na ambao alitumia kuwania urais, ndiye aliwasilisha kesi.

Marudio ya kiti cha urais yalifanyika Oktoba 26, 2017, japo Raila hakushiriki. “Si 2013 na 2017 tulitwaa serikali, hata wakati Maraga alileta kisirani na tukapata tena…Hii ya 2022 itatushinda kweli?” Ruto akataka kujua wakati akihutubia umati wa watu Shamata.

“Kuna watu wanatuambia saa hii ati sisi wote tumekosa mtu wa kutuongoza. Wameishi kutupangia uchumi kutoka juu, miaka 50 imepita, watu wa chini (akimaanisha wenye mapato madogo) wanangoja hawapati maendeleo. Mimi nasema tutaanza chini tukienda juu,” akaelezea, akipigia upatu mfumo wake wa Bottom-Up, anaotumia kufanya kampeni kutafuta uungwaji mkono.

Dkt Ruto ametangaza atawania urais kupitia UDA, chama alichozindua mwaka huu baada ya wandani wake kutimuliwa katika kamati mbalimbali bungeni. Amekuwa akikosoa Jubilee, akisema chama hicho kimekumbwa na kusheheni utapeli na kukosa demokrasia.

You can share this post!

Raila alakiwa kishujaa Nyeri akiahidi urafiki wake na jamii...

Diamond League 2022 kuanza Mei 13

T L