Ruto sasa aingia vijijini akilenga kuvumisha UDA

Ruto sasa aingia vijijini akilenga kuvumisha UDA

Na ERIC MATARA

NAIBU Rais William Ruto amejitokeza wazi na kuanza kuvumisha chama cha United Democratic Alliance (UDA) vijijini kote nchini.

Chama hicho kimeanza msururu wa mikutano kujiandaa kwa uchaguzi wa mashinani na mchujo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mikutano hiyo pia imetajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa mashinani wa Juni 2021, kuchagua maafisa wa wadi, maeneo bunge na kaunti.

Maafisa wa kitaifa watachaguliwa na wanachama wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC), baadaye mwaka huu 2021.

Mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa UDA, Bi Veronica Maina, alikutana na mamia ya wawaniaji kutoka eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa katika hoteli moja mjini Nakuru.

Taifa Leo ilifahamu kwamba mikutano hiyo itajumuisha, miongoni mwa mengine, kuelezea wawaniaji wa chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, malengo, manifesto na katiba ya chama.

“Tumezungumzia miongoni mwa mambo mengine, kueleza mfumo wa chama kufanya maamuzi, uteuzi, utatuzi wa mizozo na kanuni za chama,” alifichua Bi Maina baada ya mkutano huo.

Katibu huyo mkuu pia aliwahakikishia wawaniaji kwamba chama kitaandaa uteuzi wa haki na kwa njia ya uwazi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mkutano huo ulileta pamoja wawaniaji na viongozi kutoka kaunti za Nakuru, Baringo, Bomet, Nyandarua na Narok.

Haya yanajiri wakati chama hicho kimeanza kampeni ya kusajili wanachama wapya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika ngome ya Dkt Ruto ya Rift Valley, wanasiasa wanaomuunga mkono wanajiandaa kupigania tiketi ya chama hicho kabla ya 2022.

Wawaniaji wa viti mbali mbali vikiwemo ugavana, useneta, ubunge na wawakilishi wa wadi wanamezea mate chama hicho kipya wakilenga kukitumia kutetea viti vyao au kuwaangusha wapinzani wao hatua ambayo inaweza kusababisha migogoro kabla ya 2022.

Bi Maina alisema chama cha UDA kitaandaa mikutano sawa na wa Nakuru, huko Meru na Mombasa na maeneo mengine nchini.

“Tunaandaa mikutano katika kumbi kwa kuzingatia kanuni za kuzuia Covid-19 zilizotolewa na wizara ya afya,” alisema Bi Maina.

Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika, mwakilishi wa Kike Kaunti, Bi Liza Chelule ni miongoni mwa waliosimamia mkutano huo.

Diwani wa Wadi ya Kabazi, Dkt Peter Mbae, anayenuia kugombea kiti cha ubunge cha Subukia, aliambia Taifa Leo kwamba UDA kinabadilika kuwa chama chenye nguvu eneo la Rift Valley na kote nchini.

“UDA ndicho chama cha siku zijazo katika Rift Valley kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hii ndiyo sababu tulikutana kuweka mikakati ya siku zijazo ya chama na kuhakikisha uteuzi na uchaguzi utafanyika vyema. Kuanzia sasa, utaona wanasiasa wengi wa Rift Valley wakitaka kujiunga na UDA,” alisema Dkt Mbae.

“Katika Rift Valley, huku ndiko kuporomoka kwa chama cha Jubilee. Kwenye uchaguzi wa 2022, hii itakuwa ngome ya UDA,” aliongeza.

Tayari, vita vya ubabe vya kuthibiti chama hicho Kaunti ya Nakuru vimeshuhudiwa kati ya Seneta Kihika na mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri.

You can share this post!

Uhuru aongoza Wakenya kuomboleza Kalembe Ndile

Helikopta iliyokuwa imembeba Raila yaanguka punde baada ya...