Habari

Ruto sasa akosa matumaini kurai Weta, Mudavadi

June 30th, 2020 2 min read

BENSON AMADALA na DERICK LUVEGA

JUHUDI za wandani wa Naibu Rais William Ruto kuwashawishi; Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula kujiunga naye zaelekea kugonga mwamba baada ya kuibuka kila mmoja ana malengo tofauti kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Huku wabunge wanaomuunga Dkt Ruto wakiona mazungumzo yanayoendelezwa kama nafasi ya eneo hilo kuunga mkono azma ya Naibu Rais kugombea urais 2022, wale wanaomuunga Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wanataka Naibu Rais asaidie mmoja wao kushinda urais.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mbunge wa Mumias Mashariki Ben Washiali, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alisema wataendeleza juhudi za kurai eneo hilo kumuunga Naibu Rais.

“Ninamuunga Naibu Rais William Ruto kuwa 2022 na wakati umefika jamii ya Waluhya kuwatenga viongozi wanaotumiwa kupigia debe watu kutoka nje ya eneo hili,” alisema.

Lakini Bw Wetang’ula alisema kwamba mazungumzo yanayoendelea miongoni mwa viongozi wa Waluhya waliokataa kuunga mabadiliko yanayofadhiliwa na wanaounga handisheki hayafai kuchukuliwa kumaanisha kwamba wanamuunga Dkt Ruto.

Bw Wetang’ula alisema kwamba yeye na Bw Mudavadi wanalenga kuunganisha jamii hiyo ili iweze kumuunga mmoja wao kugombea urais 2022.

“Kuna watu wanaofikiri kwamba iwapo hauko upande wao, uko upande unaowapinga,” alisema Bw Wetang’ula.

Katika ujumbe kupitia Twitter, Bw Mudavadi alisema ripoti kwamba ataungana na Dkt Ruto ni feki.

Kauli yake ilijiri huku mbunge wa Sabatia Alfred Agoi ambaye ni mwandani wake akisisitiza kuwa viongozi hao wanazungumza na Dkt Ruto kuhusu muungano kabla ya uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa na mwenzake wa Lugari Ayub Savula alisema kwamba mazungumzo yanayoendelea ni ya kuhakikisha kiongozi wa eneo hilo atagombea urais.

Bw Wamalwa alisema jamii hiyo itafuata mwelekeo wa kisiasa wa Bw Wetang’ula na Mudavadi.

Lakini Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alisema Mudavadi na Wetang’ula wanataka jamii hiyo imuunge Dkt Ruto njama ambazo alisema hazitafaulu.

Mbunge wa Kimilili, Bw Didimus Barasa, ambaye pia ni mwandani wa Dkt Ruto alisema kuna matumaini tele kwamba mazungumzo yanayoendelea yatafanikiwa.

Kulingana naye, wahusika wanaamini hatimaye Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula watakubali kushirikiana na Naibu Rais.

“Sisi kama viongozi wa jamii ya Waluhya tumeamua kuungana kwa manufaa ya jamii yetu na taifa kwa jumla,” akasema.

Mazungumzo ya wandani wa watatu hao yaliibuka ili kuzima kampeni inayoendeshwa na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambao wamekuwa wakizuru eneo hilo baada ya kutajwa kuwa wasemaji wa jamii ya Waluhya mwezi jana, hatua ambayo haikufurahishwa kambi za Mudavadi na Wetangula.

Bw Wamalwa na Oparanya, ambao walikamilisha mikutano yao ya kisiasa kaunti ya Kakamega Jumamosi, wametembelea kaunti za Bungoma, Busia na Vihiga wakiahidi jamii kwamba serikali itakamilisha miradi ya maendeleo eneo hilo.

Walikutana na wazee kutoka jamii ya Waluhya katika juhudi za kubadilisha siasa za eneo hilo ambazo zimekumbwa na mgawanyiko.

Lakini wandani wa Dkt Ruto, Bw Mudavadi na Bw Wetangula wanasema kwamba kuna njama za kushawishi eneo hilo kumuunga kiongozi wa ODM Raila Odinga.