Habari

Hamuwezi kuwa na nguvu sawa na za Muumba, Ruto aambia wanaopinga michango maabadini

June 29th, 2019 2 min read

Na SHAABAN MAKOKHA

NAIBU Rais William Ruto amefanya ziaran mjini Mumias, eneo la Magharibi ambapo amehudhuria sherehe za kila mwaka za Familia kutoa shukrani na Sadaka Takatifu katika Dayosisi ya Mumias ya Kanisa la Anglikana na kuwataka baadhi ya wanasiasa wanaopinga michango ya kanisani kukoma kujihisi ni kama wana nguvu sawa na za Mwenyezi Mungu.

Dkt Ruto alikuwa ameambatana na wabunge John Waluke (Sirisia), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) Johnson Naicca (Mumias Magharibi), Eric Muchangi (Runyenjes), Charles Njagagwa (Mbeere Kaskazini), na viongozi Boni Khalwale (aliyekuwa Seneta Kakamega), na Rashid Echesa (aliyekuwa Waziri wa Michezo), miongoni mwa viongozi wengine.

Ziara hii inakuja wiki mbili baada ya Ruto kuzuru eneo hili alipoongoza mchango kwa kanisa la African Divine Church (ADC) Chebuka kaunti ya Vihiga.

Naibu Rais alianza kwa kukata utepe kuashiria uzinduzi wa msingi wa ujenzi wa Bishop Hanington Training & Recourse Centre; kituo ambacho kitagharimu kiasi cha Sh64 milioni.

 

Naibu Rais William Ruto akipokelewa na Askofu Joseph Maumo Wandera wa Dayosisi ya Mumias ya ACK Jumamosi, Juni 29,  2019. Picha/ Isaac Wale

Ruto amesaidia kuchangisha Sh11.3 milioni kama sehemu ya jumla ya Sh64 milioni hizo.

Naibu Rais ametoa Sh1 milion na Sh500,000 kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Amerudia tamko lake la kuwashambulia baadhi ya viongozi wanaopinga michango kanisani kutoka kwa wanasiasa.

“Pendekezo hilo la kuwafungia nje wanasiasa wanaotaka kutoa michango kanisani haliwezi kufanya kazi Kenya kwa sababu ni taifa lililoundwa kwa msingi wa kufuata dini na Wakenya wanatambua uwepo wa Mungu,” amesema Ruto.

Amewataka wanasiasa wakome kujifananisha na Mungu kwa sababu “wataangamia vibaya.”

Mbunge Muchangi wa Runyenjes amesema mswada wa kupinga pesa za wanasiasa kanisani ukiwasilishwa bungeni utaanguka mara iyo hiyo.

“Mswada huo nawaambia utaanguka kwa sababu sisi ni watu wanaomtambua Mwenyezi Mungu,” amesema Muchangi ambaye ni mmojawapo wa wabunge vijana zaidi.

Muchangi amesema viongozi wanaopinga michango kanisani hata wengi wao hajaeleza Wakenya waziwazi ni dini au imani gani wanafuata.

Naye mwenyeji wao, mbunge Johnson Naicca wa Mumias Magharibi amemtaka Naibu Rais kujaribu awezavyo kuhakikisha serikali inasaidia kufufua kiwanda cha Sukari cha Mumias.

“Zungumza na Rais Kenyatta vizuri ahakikishe kinaanza kusaga miwa kutengeneza sukari; ukifanikiwa tayari utakuwa na kura za watu wa eneo hili,” amesema Naicca.