Michezo

Rutto na Kitur kushiriki katika Mumbai Marathon

January 14th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Mumbai Marathon, Evans Rutto (2014) na Bornes Kitur (2017) wako katika orodha ya wakimbiaji 46,000 watakaoshiriki makala ya 16 ya mbio hizi za kimataifa nchini India hapo Januari 20, 2019.

Rutto, 34, ameapa kurejesha taji lake akisema huenda atahitajika kuvunja rekodi ya Mumbai Marathon ya wanaume ya saa 2:08:35, ambayo Mkenya mwenzake Gideon Kipketer anashikilia tangu mwaka 2016.

“Nahisi niko sawa kabisa kurejesha taji langu na huenda nikahitajika kuandikisha rekodi mpya ya mbio hizi kupata ufanisi huo,” alinukuliwa na gazeti la Times of India akisema.

Wapinzani wa Rutto wakali ni Waethiopia Solomon Deksisa (bingwa mtetezi), Chele Dechasa na Abraham Girma na mzawa wa Ethiopia, Shumi Dechasa, ambaye ni raia wa Bahrain, pamoja na Mkenya Joshua Kipkorir, ambaye aliridhika katika nafasi ya pili mwaka 2018.

Rekodi ya wanawake ya Mumbai Marathon ya saa 2:24:33, ambayo Mkenya Valentine Kipketer anashikilia tangu mwaka 2013, pia itakuwa hatarini kuvunjwa.

Kitengo hiki kimevutia Mkenya Kitur pamoja na Waethiopia Amane Gobena na Shuko Genemo ambao walitwaa mataji ya mwaka 2018 na 2016, mtawalia.

Kutoka orodha ya 46, 000 ni 8, 414 pekee ndio watashindana katika mbio za kilomita 42, huku waliosalia wakitimka katika mbio za kilomita 21 na kilomita 10.