Habari

Ruweida Obbo ashajiisha wanawake Lamu kuwa mstari wa mbele kuwania nyadhifa

October 15th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Lamu katika Bunge la Kitaifa, Bi Ruweida Obbo, amewapa motisha akina mama eneo hilo kugombea nyadhfa za juu zaidi katika uongozi wakati wanaamua kujitosa kwenye ulingo wa siasa miaka ijayo.

Bi Obbo anasema akina mama wengi eneo la Lamu wamekuwa na uoga wa kugombea nyadhifa anazoziita kubwakubwa, ikiwemo ubunge, useneta na ugavana.

Badala yake, akina mama hao wamekuwa wakikimbilia kugombea kiti cha mwakilishi wa wanawake na kile cha udiwani.

Akizungumza mjini Lamu, Bi Obbo alisema wakati umewadia kwa wanawake eneo hilo kuamka kutoka usingizi na kuwa tayari kung’ang’ania viti vikubwa vya kisiasa nchini.

Alisema anafahamu kuwa baadhi ya viongozi wanaume eneo hilo wamekuwa wakipiga vita harakati za akina mama kuongoza lakini akawashauri wote wenye nia hiyo kutotishwa.

“Tusiwe tu kila mara uchaguzi unapowadia tunakimbilia kutafuta nafasi ya uwakilishi wa wanawake au udiwani ambao ninasema ni rahisi kuupata. Tuwe mstari wa mbele kugombea viti vya ubunge, useneta na hata ugavana. Najua ninaposema hivyo baadhi ya wanaume hukereka na hata kunipiga vita. Ushauri wangu ni kwamba tusikubali kutishwa au kuvunjwa moyo na yeyote. Tuwe imara na tujitose kwenye kinyang’anyiro cha viti vyote, ikiwemo kile chga ugavana,” akasema Bi Obbo.

Changamoto

Baadhi ya wanawake waliozungumza na Taifa Leo aidha walikiri kukumbwa na changamoto tele kila mara wanapojitosa siasani.

Bi Amina Bunu anasema jamii ya Lamu yenyewe haijatoa kipaumbele na uhuru kwa mwanamke kuongoza.

“Jamii yetu iko na taasubi ya kiume. Hii ndiyo sababu unaposimama kugombea nyadhfa za kisiasa, watu huanza kukuangalia kwa jicho baya. Wanakuona wewe kuwa mtovu wa maadili. Hata wanawake wenzetu wenyewe pia hutuangusha kwa kutuponza,” akasema Bi Bunu.

Kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa Agosti 8, 2017, kiti cha ugavana na kile cha useneta vilikosa wagombea wowote wa jinsia ya kike aghalabu Lamu.

Kati ya wagombea wanane wa kiti cha ubunge eneo la Lamu Magharibi, ni wagombea watatu pekee ndio waliokuwa wa jinsia ya kike.

Eneo la Lamu Mashariki, wagombea wote wanne waliojitokeza kutafuta kiti hicho cha ubunge walikuwa wanaume.