Makala

Ruweida Obbo: Simba jike wa Lamu anayempa mtoto wa kike matumaini

April 29th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

USEMI uvumao katika ulimwengu wa sasa wa ‘awezacho kukifanya mwanamume, mwanamke anaweza kukifanya hata zaidi’ unadhihirishwa wazi na Mbunge wa Lamu Mashariki, Bi Ruweida Obbo.

Bi Obbo, maarufu kama ‘Captain Ruweida,’ ni kiongozi anayetambulika, si eneobunge lake la Lamu Mashariki analowakilisha pekee bali pia kaunti nzima na Pwani.

Ni mbunge shupavu ambaye wengi Lamu wanamtambua kama ‘Simba Jike’ kutokana na ukakamavu wake katika kuyajadili na kuyakemea mambo vile yalivyo pasi na kuogopa chochote.

Akitokea jamii ya Waswahili wa asili ya Kibajuni ambayo tangu jadi imetambulika kwa kutompa kipaumbele mtoto wa kike, hasa kielimu, Bi Obbo amekuwa kielelezo cha mtoto msichana eneo hilo huku akiwapa matumaini kwamba wanaweza.

Ndiye mwanamke wa kwanza Mbajuni kutoka Lamu kusomea na kuhitimu kozi ya urubani.

Bi Obo kwa sasa ni mweledi wa kuendesha ndege, hatua iliyopelekea yeye kubandikwa jina lake la ‘Captain Ruweida.’

Kila kuchao, Bi Obbo anaendelea kutoa changamoto, hasa kwa jinsia ya kike, akiihimiza jamii yake kuhakikisha wasichana kwa wavulana wanapewa nafasi sawa kimasomo na masuala mengine ya kimsingi na maendeleo.

Mbali na kuitetea jinsia ya kike, Bi Obbo pia amekuwa mstari wa mbele kukemea maovu, hasa dawa za kulevya kaunti ya Lamu.

Vijana wengi eneo hilo wamegeuzwa kuwa goigoi na dawa za kulevya, hali ambayo wa Lamu wanahisi imegeuka kuwa janga.

Huku viongozi wengine wa Lamu, ikiwemo wale wa jinsia ya kiume mara nyingi wakiogopa kuligusia suala hilo la mihadarati kutokana na uzito wake kulihusu, Bi Obbo kwa upande wake haogopi kulisema, kufoka au kukemea suala hilo nyeti hata kukiwa na vitisho vya aina yoyote kutoka kwa wahusika wa biashara hiyo haramu ya dawa za kukevya.

Kuna wakati ambapo Bi Obo amewahi kukiri mwenyewe kwamba licha ya vidudu watu wanaoendeleza kichinichini usambazaji na uuzaji wa dawa za kulevya na kuharibu jamii ya Lamu kumrushia vitisho vya mara kwa mara,yeye katu hatarudi nyuma katika kukemea uovu huo ilmradi jamii,hasa vijana wa Lamu wapone.

“Vijana wetu wameharibiwa na dawa za kulevya.Wamekuwa goigoi bila ya faida yoyote kwa jamii. Hawa wauzaji dawa za kulevya ni wauaji. Kwa sababu hiyo, ningeomba idara ya usalama kuja na mfumo wa kuwapiga risasi na kuwaua papo hapo washukiwa wa dawa za kulevya wanaopatikana mitaani badala ya kuwashika na kuwapeleka kortini. Kwa sababu wanajiweza kisenti, siku chache baadaye utawapata wameachiliwa kwa dhamana, hivyo kurudi mitaani kuendeleza biashara yao ya mihadatati na kuharibu vijana wetu,” akasema Bi Obbo.

Mbunge huyo pia anafahamika Lamu na Pwani kwa misimamo yake mikali katika kuwatetea watoto wasichana wasidhulumiwe.

Amewahi kuwafokea maafisa wa usalama, hasa wale wanaoendeleza operesheni ya kiusalama ya kuwaska magaidi wa Al-Shabaab Lamu na msitu wa Boni kwa kujihusisha kingono na wasichana wadogo eneo hilo.

Kuna wakati ambapo Bi Obbo alikodisha ndege ya kwenda eneo la Kiunga lililoko mpakani mwa Kenya na Somalia, ambapo aliwaokoa wasichana waliokuwa wakinyanyaswa kingono na walinda usalama.

Ni kutokana na juhudi zake ambapo visa vilivyokuwepo vya maafisa wa usalama kushiriki ngono na watoto wa shule eneo hilo la Lamu Mashariki vimepungua pakubwa.

Kwa wakati mmoja, Bi Obbo aliahidi kuwasilisha mswada bungeni wa kutaka wote watakaopatikana wakishiriki ngono, kunajisi au kuchafua wasichana wadogo wahasiwe (castrated) badala ya kukamatwa na kushtakiwa.

“Sioni sababu ya kumkamata mchafuzi wa watoto na kisha eti unampeleka mahakamani wakati akiwa amempachika mimba au kuharibu maisha au ndoto ya mtoto wa kike. Adhabu nzuri ni wanaume wanaopatwa na makosa hayo wahasiwe au kukatwa huo uume. Hilo litawafanya wanaume hao baada ya kutoka jela wasiwe na fikra au uwezo tena wa kuharibu hawa mabinti zetu,” akasema Bi Obbo.

Bi Obbo pia amekuwa akiipigania vilivyo jamii yake ya Wabajuni ili kujinasua kutoka kwa dhuluma za kihistoria, ikiwemo suala la umiliki wa ardhi kwa wenyeji kindakindaki wa Lamu.

Utelekezaji wa kimaeneo, hasa Lamu Mashariki, kimaendeleo ambao umekuwa ukiendelezwa na utawala wa serikali zilizopita nchini Kenya pia ni jambo ambalo Bi Obbo hajalinyamazia.

Kila anaposimama majukwaani utamsikia akifoka kwamba wakazi halisi wa Lamu wapewe ardhi na hatimiliki kwani wao pia wana haki kama Wakenya wengine.

Anataja utelekezaji wa jamii yake ya Wabajuni kuwa jambo linalovunja moyo na kuwakosesha wananchi imani.

Anasema ni huo huo utelekezaji wa maeneo ambao ndio unaochangia kukosekana kwa usalama, hasa Lamu Mashariki.

“Wananchi wamechoka. Tangu uhuru wa nchi hii kupatikana, hakuna mradi wa kimsingi ambao wananchi wa Lamu Mashariki wanaweza kujivunia isipokuwa ule wa ujenzi wa barabara ya Mtangawanda-Kizingitini uliozinduliwa mwaka jama na Rais wetu, William Ruto. Ipo haja ya miradi zaidi kutekelezwa eneo hili,” akasema Bi Obbo.

Mbunge huyo pia amekuwa akifuatana unyounyo na walinda usalama, hasa wale wanaotekeleza operesheni msitu wa Boni katika harakati za kuhakikisha watu wake wa Lamu Mashariki na kaunti nzima kwa jumla wanapata usalama na amani ya kudumu kama sehemu zingine zozote za Kenya.

“Twataka kuona serikali ikiongeza nguvu hivi vita dhidi ya magaidi ili Lamu ifurahie kuwa eneo bora la kuishi na kutekelezea maendeleo,” akasema.

Ni kupitia uongozi wa Bi Obbo, ambapo visiwa vingi vya Lamu Mashariki vimeweza kuunganishwa kwa umeme miaka ya hivi karibuni.

Itakumbukwa kuwa Julai, 2020, Bi Obbo aliongoza mamia ya wananchi kwenye maandamano ya siku tatu mfululizo, mchana na usiku, ambapo kwa pamoja walilala kwenye uwanja wa ofisi za kampuni ya usambazaji umeme (KPLC) mjini Faza, hivyo kupelekea stima kuunganishwa au kurudishwa isikatwekatwe tena hadi wa leo.