Rwanda kufungua mpaka na Uganda

Rwanda kufungua mpaka na Uganda

NA MASHIRIKA

KIGALI, RWANDA

SERIKALI ya Rwanda imesema itafungua tena mpaka wake na Uganda mwezi huu huku ikijitahidi kuzima taharuki kati ya nchi hizo mbili jirani.

Kituo cha mpakani cha Gatuna/Katuna na vinginevyo vitafunguliwa kuanzia Januari 31, 2022 kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Masuala ya Kigeni na Ushirikiano Kimataifa.

“Kufuatia ziara ya Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mshauri Mkuu wa Rais kuhusu Operesheni Maalum na Kamanda wa Vikosi vya Nchi Kavu vya Jeshi la Uganda People’s Defence Forces (UPDF) mnamo Januari 2022, serikali ya Rwanda imethibitisha kuwa kuna mchakato wa kusuluhisha masuala yaliyotajwa na Rwanda, pamoja na ahadi iliyotolewa na Serikali ya Uganda kuangazia masuala yaliyosalia. Kutokana na jambo hili na kuambatana na majadiliano katika awamu ya nne ya Kongamano Kuu lililofanyika Gatuna/Katuna Februari 21, 2020, serikali ya Rwanda ingependa kufahamisha umma kuwa mpaka wa Gatuna kati ya Rwanda na Uganda utafunguliwa kutoka Januari 31, 2022,” ilisema taarifa hiyo iliyochapishwa Ijumaa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Uhusiano uliovurugika kati ya mataifa hayo mawili yanayokaribiana na nchi za Afrika Mashariki ulisababisha Rwanda kufunga mpaka wa Katuna/Gatuna mnamo Februari 2019.

“Sawa na ilivyo kuhusu vituo vinginevyo vya mpakani nchini, Wizara za afya nchini Rwanda na Uganda zitashirikiana kuweka mikakati inayohitajika kuwezesha usafiri kuhusiana na Covid-19,” ilisema.

Rwanda ilisema bado imejitolea kufanikisha juhudi zinazoendelea za kusuluhisha masuala yaliyosalia kati yake na Uganda na inaamini kuwa kufungua mpaka tena kutachangia kwa njia chanya kurejesha haraka mahusiano mema kati ya nchi hizo mbili.

Kulingana na Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, Adonia Ayebare, hatua ya kufungua tena mpaka ni ishara kuu kwa “watu wa nchi hizo mbili.”

“Hii inamaanisha mengi kwa watu wa nchi hizi mbili. Pongezi kwa hatua hii muhimu ya kurejesha mahusiano thabiti ya kibiashara kati ya mataifa haya mawili,” aliandika Bw Ayebare kwenye Twitter mnamo Januari 17, 2022, alipowasilisha ujumbe huo maalum kutoka kwa Rais Museveni kwa Rais Kagame kabla ya ziara ya Jenerali Kainerugaba.

Saa kadhaa baada ya ziara yake wikendi nchini Rwanda, Jenerali Kainerugaba anayekisiwa kuwa huenda akawa mrithi wa babake mwenye umri wa miaka 77, Rais Museveni, alisema alishiriki “mazungumzo ya kirafiki mno” na ya kina kuhusu jinsi ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo jirani.

“Nina hakika kuwa chini ya uongozi wa marais wetu wawili tutaweza kurejesha haraka mahusiano yetu bora ya tangu jadi,” alisema Kamanda huyo wa zamani wa SFC.

Mkutano huo uliofanyika siku kadhaa baada ya Kainerugaba kuchapisha kwenye Twitter picha mbili za Kagame, moja akiwa kijana akiwa amevalia magwanda ya kijeshi na nyingine ya majuzi akiwa amevalia suti.

“Huyu ni mjomba wangu Paul Kagame. Wanaopigana naye wanapigana na familia yangu. Wote wanapaswa kujihadhari,” ulisema ujumbe huo.

Museveni, babake Kainerugaba na Rais Kagame walikuwa marafiki wa karibu katika miaka ya 1980 na 1990 wakati nchi zao mtawalia zilikuwa zikipigania uhuru kabla ya kugeuka kuwa mahasimu wakuu.

Rwanda ilifunga ghafla mpaka wake na Uganda mnamo Februari 2019, na kukata mkondo muhimu wa biashara.

Taifa hilo lilishutumu Uganda dhidi ya kuwateka nyara raia wake na kuunga mkono waasi waliotaka kumng’oa mamlakani Kagame.

Kwa upande wake, Uganda iliishutumu Rwanda dhidi ya upelelezi pamoja na kuwaua wanaume wawili ilipovamia ardhi ya Uganda 2019 dai linalokanushwa na Kigali.

You can share this post!

Zaidi ya 70 wauawa na kimbunga Ana

Kaunti yataka miili ipelekwe mochari Nairobi

T L