Michezo

Rwanda kukosa huduma za Tuyisenge AFCON

September 6th, 2018 2 min read

Na Geoffrey Anene

AMAVUBI ya Rwanda imepata pigo kubwa kabla ya mechi yake ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 dhidi ya Ivory Coast hapo Septemba 9, 2018 baada ya ripoti nyota Jacques Tuyisenge atakuwa shabiki tu kutokana na jeraha la shingo.

Kwa mujibu wa gazeti la New Times nchini Rwanda, mshambuliaji huyu matata wa Gor Mahia alikuwa muhimu sana katika kampeni ya Amavubi kwenye Soka ya Afrika ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao (CHAN) mwaka 2016. Alichangia pakubwa katika mechi ya ufunguzi, ambayo nchi yake ililemea Ivory Coast 1-0.

Kocha Vincent Mashami, gazeti hilo limesema, amekiri ni pigo kubwa kwa Rwanda kukosa huduma za Tuyisenge inapojiandaa kukaribisha Elephants ya Ivory Coast kwa mchuano huu wa Kundi H, ambalo pia linajumuisha Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Guinea Conakry.

Tuyisenge, ambaye alijiunga na Gor mnamo Februari mwaka 2016 kutoka Police FC nchini Rwanda, aliumia shingo katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederation Cup) kati ya Gor na miamba wa Rwanda, Rayon Sports mnamo Agosti 19.

“Alishauriwa na madaktari wa klabu yake asisakata soka kwa muda baada ya kufanya jeraha lake kuwa baya zaidi dhidi ya USM Alger nchini Algeria mnamo Agosti 29,” gazeti hilo limesema.

Katika msimu wa Gor mwaka 2018, Tuyisenge amepachika mabao 13 kwenye Ligi Kuu na kuona lango mara tatu katika Caf Confederation Cup. Gor ilihifadhi ubingwa wa Ligi Kuu zikisalia mechi sita, ingawa ilifungiwa nje ya robo-fainali ya Confederation Cup baada ya USM Alger na Rayon kufuzu kutoka Kundi D.

Jereha hilo la shingo linatisha kuondoa Tuyisenge katika vita vya kuwania tuzo ya mfungaji bora ligini. Zikisalia mechi tano ligi itamatike, Tuyisenge anahitaji mabao mawili kumfikia Elvis Rupia wa Nzoia Sugar. Mshambuliaji wa zamani wa Gor, Meddie Kagere, ambaye sasa ni mali ya Simba SC nchini Tanzania, ni mmoja wa silaha Rwanda itategemea kupata matokeo mazuri dhidi ya Ivory Coast.