Michezo

S8PL: Mathare Flames kwa mara ya kwanza yaichoma Metro

April 16th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE 

MATHARE Flames iliinyamzisha Metro Sports huku Jericho Allstars ikiirarua Kawangware United kwa mabao 4-1 na kuendelea kukaa kileleni katika uwaniaji wa Super Eight Premier League (SP8 PL).

Jacob Bashir alipiga bao moja safi na kuisadia Mathare Flames kubeba ushindi wa kwanza dhidi ya Metro Sports baada ya kutoka nguvu sawa mara mbili mwaka 2018.

Makabiliano ya wachezaji wa Metro Sports na mmoja wa Mathare Flames kwenye mechi ya Super Eight Premier (S8PL) uIliyopigiwa Uwanja wa Drive Inn, Mathare Nairobi. Mathare ilishinda kwa bao 1-0. Picha/ John Kimwere

Mabingwa watetezi, Jericho Allstars ambayo inafunzwa na kocha Thomas Okongo iliendelea kuimarisha kampeni zake na kuweka mwanya wa alama tatu mbele ya Lebanon FC.

”Ninashukuru vijana wangu wanafanya kazi nzuri. Wanajituma kwenye jitihada za kutetea taji hilo tuliloshinda msimu uliyopita,” kocha wa Jericho Allstars, Thomas Okongo alisema na kuongeza kuwa wanalenga kuponda Lebanon ili kupanua nafasi yao kwenye jedwali.

Nayo Team Umeme ilijipata njia panda ilipozaba kwa mabao 2-1 na Rongai Allstars ikiwa ni baada ya kuyeyusha alama tatu wiki iliyopita.

Kwenye matokeo mengine, NYSA inaonekana inahitaji kazi makubwa maana inazidi kusuasua kwenye mechi hizo msimu huu. NYSA ilikubali kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Huruma Kona kupitia Johnson Adesoji aliyetikisa wavu mara mbili huku Peter Ng’ang’a akitingia NYSA bao la kufuta machozi.

Matokeo ya mechi za wikendi iliyopita

Huruma Kona                      2-1     NYSA
Mathare Flames                  1-0     Metro Sports
Rongai Allstars                    2-1     Team Umeme
Melta Kabiria                       2-2    Lebanon
TUK                                       2-1     MASA
Makadara Junior L.S.A     1-4     Dagoretti Former Players FC