Uchaguzi kuzima nyota za wanasiasa maarufu

Uchaguzi kuzima nyota za wanasiasa maarufu

NA CHARLES WASONGA

MATOKEO ya Uchaguzi Mkuu wa Jumanne yatakuwa pigo kubwa kwa wanasiasa wa mrengo utakaopoteza urais.

Baadhi ya wanasiasa wa mrengo utakaopoteza watalazimika kustaafu kutoka kwenye ulingo wa siasa au kuishiwa na ushawishi wa kisiasa katika ngome zao.

Rais Uhuru Kenyatta na mgombea urais wa Azimio, Raila Odinga wanaongoza orodha ya vigogo wa Azimio ambao wameshikilia roho zao mikononi huku zikisalia saa 48 kabla ya Wakenya kuelekea debeni.

Wengine ambao watakuwa hatarini kisiasa endapo Naibu Rais William Ruto atamshinda Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais ni; mgombea mwenza Martha Karua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, na gavana wa Kitui Charity Ngilu.

Kwa upande mwingine, endapo Bw Odinga ataibuka mshindi, Dkt Ruto na Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ndio wataathirika zaidi kisiasa, katika mrengo wa Kenya Kwanza.

Rais Kenyatta anahofia kupata aibu kubwa zaidi endapo Dkt Ruto atatangazwa mshindi katika kinyang’anyiro cha urais.

Rais amekuwa katika mstari wa mbele kumpigia debe Bw Odinga, kama anayefaa kuwa mrithi wake na kuendeleza miradi ya maendeleo aliyoanzisha.

Katika muda wa wiki moja iliyopita, Rais Kenyatta amezuru karibu kaunti 10 akitumia shughuli za ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo kama majukwaa ya kumpigia debe Odinga.

Wadadisi wa kisiasa wanasema Rais Kenyatta atapoteza masilahi ya kisiasa na kibiashara endapo Dkt Ruto ataibuka bingwa katika kinyang’iro cha urais.

“Kwanza, Rais ni mwenye hofu kuu kwa kuwa ushindi wa Dkt Ruto utakuwa pigo kwake kisiasa kwa sababu yeye ndiye mwenyekiti wa baraza kuu la Azimio. Hofu nyingine inatokana na masilahi yake ya kibiashara ambayo huenda yakaporomoka kwa kukosa mlinzi mwenye ushawishi serikali,” anasema Bw Martin Andati.

Mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa anaongeza kuwa, hali hiyo inachangiwa na kuzorota kwa uhusiano kisiasa kati yake na Dkt Ruto alipomtelekeza na kumkumbatia Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018.

“Hofu kuu ya Rais Kenyatta ni kwamba, hatakuwa salama chini ya Dkt Ruto kama Rais wa Kenya kwa kumsaliti alipovunja ahadi ya kumuunga mkono (Dkt Ruto) baada ya kukamilisha mihula yake miwili mamlakani,” Bw Andati anaeleza.

Kwa upande wa Bw Odinga, wadadisi wanasema kushindwa kwake kutakuwa mwisho wa ushawishi wake kisiasa ikizingatiwa umri wake ni mkubwa.

“Hofu ya Bw Odinga ni kwamba, Dkt Ruto akimshinda, ataelekea Bondo kupumzika kwa sababu uzee umemlemea. Mnamo 2027 atakuwa na umri wa miaka 82 na bila shaka hatawania kiti chochote,” anasema Wakili Kipchumba Karori.

Naye Bi Karua, 64, yuko roho mkononi kwa sababu tangu 2009 alipojiuzulu kutoka serikali ya rais wa zamani Mwai Kibaki, hajawahi kuwa serikalini.

Kwa hivyo, ushindi wa Dkt Ruto na Rigathi Gachagua utazika kabisa ndoto yake, sio tu ya kurejea serikalini bali kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa Naibu Rais.

Bw Musyoka, 68, pia ni mwenye wasiwasi tele kwani ushindi wa Dkt Ruto utamrejesha katika baridi ya kisiasa ambayo imemsokota kwa miaka 10, tangu 2013.

Alihudumu kama makamu wa rais chini ya marehemu Kibaki kati ya 2007 na 2013.

Aidha, amekuwa mgombea mwenza wa urais wa Bw Odinga katika chaguzi za 2013 na 2017 lakini wakashindwa na Rais Kenyatta.

Katika Azimio, Bw Musyoka ameahidiwa wadhifa wa Waziri Mkuu endapo Bw Odinga atashinda.

Bi Ngilu, 70, pia ni mwingi wa wasiwasi kwa sababu mwezi Julai, alikubali kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kutetea kiti chake kwa ahadi ya kuteuliwa Waziri Bw Odinga akishinda.

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti, 54, ni mwingi wa wasiwasi kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kwamba, atapigwa kalamu endapo Dkt Ruto atafaulu kuingia Ikulu.

Na endapo Bw Odinga atashinda urais, inavyobashiriwa katika matokeo ya kura za maoni, Dkt Ruto atapoteza kabisa ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba, Bi Karua kama Naibu Rais, kwa usaidizi wa Bw Kenyatta kama Rais mstaafu watawavutia wabunge watakaoingia bunge kwa tiketi ya UDA,” anasema Bw Andati.

Japo, Bw Ruto mwenye umri wa miaka 55, anaweza kuwania urais kwa mara nyingine 2027, inakisiwa kuwa ushawishi wake utakuwa umepungua pakubwa.

“Dkt Ruto pia hatakuwa na nguvu za kifedha alizonazo wakati huu,” anasema.

Jumanne, Wakenya watachagua viongozi 1,882 kati ya wawaniaji 16,098 wanaotafuta viti kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.

Wawaniaji 14,216 wataambulia patupu licha ya kutumia mamilioni katika kampeni.

Kipindi cha kampeni kinakamilika leo Jumamosi jioni.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati jana Ijumaa alisema kuwa shehena ya mwisho ya karatasi za kupigia kura itawasili humu nchini kesho Jumapili.

  • Tags

You can share this post!

Wanaodaiwa kusambaza ujumbe wa uchochezi wapata bondi

Zelensky ashutumu shirika la Amnesty kwa kutuhumu wanajeshi...

T L