Saba wafariki kwenye ajali matatu zilipogongana Kaunti ya Kilifi

Saba wafariki kwenye ajali matatu zilipogongana Kaunti ya Kilifi

MAUREEN ONGALA na WACHIRA MWANGI

WATU saba walifariki katika ajali ya barabarani usiku wa kuamkia jana, Kaunti ya Kilifi.

Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa moja unusu eneo la Roka, barabara kuu ya Kilifi-Malindi, ilisababisha vifo vya watu wanne papo hapo, na wengine wakafariki walipofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi.

Kamanda wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini, Bw Jonathan Koech, alisema uchunguzi wa kwanza uliashiria matatu zilizogongana zilikuwa zinaendeshwa kwa kasi.

“Ajali ilihusisha magari mawili ya uchukuzi wa umma. Moja lilikuwa linaelekea Mombasa kutoka Malindi na lingine lilikuwa linatoka Kilifi kuelekea Malindi. Imeonekana matatu iliyokuwa ikitoka Malindi ilikuwa inajaribu kupita gari lingine kwa kasi ndipo ajali ikatokea,” akasema.

Baadhi ya waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi kwa matibabu. Waliofariki ni watoto wawili, wanawake watatu na wanaume wawili.

Kwingineko, mfanyakazi wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) alifariki mjini Mombasa baada ya kuvamiwa na nyuki ndani ya gari alimokuwa akisafiria pamoja na watu wengine wawili.

Kulingana na polisi, Bw John Muthine Mutwiri, alikuwa akiendesha gari hilo katika barabara ya Jomo Kenyatta mnamo Jumamosi asubuhi, wakati nyuki walipoingia ghafla.

“Walishuka kwa gari kutafuta usalama nje na kila mmoja akakimbia upande tofauti. Dereva alizidiwa nguvu akaanguka katika gereji ambalo lilikuwa karibu. Mwenye gereji hilo aliita tuktuk na kumkimbiza hospitalini lakini madaktari wakathibitisha alikuwa amefariki,” ripoti ya polisi ilieleza.

Katika ujumbe wa rambirambi kwa familia, Kamishna wa kitengo cha Upelelezi na Usalama katika KRA, Dkt Edward Karanja, alithibitisha kuwa marehemu alikuwa akihudumu katika kitengo hicho Mombasa.

“Tunaombea familia yake, marafiki na wafanyakazi wenzake faraja wakati huu mgumu,” akasema kwa taarifa.

Shughuli za kawaida zilisitishwa kwa muda katika eneo hilo pale watu waliokuwa karibu walipokimbia ili kuepuka kuumwa na nyuki hao ambao bado haijabainika walikuwa wametoka wapi.

You can share this post!

Mradi wa maji kuimarisha maisha ya wakulima Gatundu

Kinara wa UoN kusomewa hukumu Januari 22 kwa kuidharau...

T L