Kimataifa

Saba wauawa raia wa Sudan wakianza upya maandamano

July 2nd, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

WATU saba waliuawa wakati maelfu ya raia walijitokeza kushiriki maandamano ya kushinikiza baraza la kijeshi linaloongoza Sudan kuachia viongozi wa kutoka upande wa raia mamlaka.

Hayo yalikuwa maandamano ya kwanza ya halaiki tangu wanajeshi walipovamia waandamanaji na kuua zaidi ya 100, ishara wazi kuwa nguvu za raia mitaani bado zipo.

Kulingana na ripoti ya wizara ya afya nchini humo, watu saba walithibitishwa kufariki na wengine 181 wakajeruhiwa.

Ripoti hiyo, hata hivyo, haikueleza kilichowaua waliokufa, wala walikuwa akina nani.

Maafisa 10 wa kijeshi walijeruhiwa katika matukio hayo, baada ya kupigwa risasi.

Maandamano hayo yalikuwa yametarajiwa kuonyesha nguvu za upinzani.

Katika maandamano ya Jumapili, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya waandamanaji waliokuwa wakielekea katika kasri la Rais.

“Tunawataka watu walioko jiji kuu kwenda katika kasri kutafuta haki kwa waliouawa na kudai kupokezwa mamlaka kwa raia,” muungano wa wataalamu Sudan (SPA) ukasema katika ukurasa wa Twitter.

Polisi vilevile walikabiliana na waandamanaji katika wilaya za Bahri, Mamura na Arkweit.

Walioshuhudia walisema waandamanaji walikuwa wakiimba kuwa wanataka uongozi wa kiraia.

“Tumechoshwa na jeshi. Kwa miongo nchi hii imeongozwa na jeshi na halikufanikiwa, halitafanikiwa hata sasa. Licha ya walichofanya kwa kuua waandamanaji, vijana hawatakoma kuendelea kupigana,” akasema Nada Adel, mwandamanaji.

Majeraha

Kundi la madaktari wanaohusishwa na waandamanaji hao awali lilikuwa limesema kuwa watu watano waliuawa mchana na wengine kujeruhiwa vibaya kwa risasi walizopigwa na wanajeshi.

Naibu mkuu wa baraza la kijeshi ambalo linaongoza, alisema kuwa wavamizi waliwapiga risasi wanajeshi wa tatu pamoja na raia sita eneo la Omdurman.

Watu waliokuwa wakipeperusha bendera za Sudan na mabango ya kuonyesha ushindi walimiminika mitaa ya Al-Sahafa, mji jirani na Khartoum.

“Hakuna aliyelipa baraza la kijeshi mamlaka, watu wote hawalitaki,” akasema mwandamanaji mwingine.

Maelfu pia waliandamana katika miji ya Port Sudan, Al-Obeid, Madani na Khasma el-Girba.